SHERIA NGOWI TOKA TANZANIA NDIYE ALIYEMVALISHA RAIS WA ZAMBIA


Mbunifu wa mavazi wa kimataifa, Sheria Ngowi ameendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania kupitia kipaji chake cha ubunifu wa mavazi baada ya kumvalisha Rais mpya wa Zambia, Edgar Lungu katika sherehe za kuapishwa kwake jana asubuhi katika viwanja vya National Heroes, mjini Lusaka-Zambia.
 
 Rais Lungu 58, aling’arisha sherehe hizo baada ya kuvaa suti rasmi (Presidential suit) rangi ya bluu, shati jeupe na tai nyekundu zilizobuniwa na Mbunifu wa mavazi wa kimataifa, Sheria Ngowi. Lungu aliambatana na mke wake, Eshter Lungu walipokuwa wanaingia viwanjani hapo huku wakisindikizwa na ulinzi mkali.
 
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Sheria Ngowi alisema amefurahi kupata nafasi ya kipekee ya kumvalisha Rais Lungu katika sherehe za kuapishwa kwake na kusema ni hatua kubwa katika kazi yake kama mbunifu wa mavazi wa kimataifa.
 
“Hii ni hatua kubwa katika kazi yangu ya ubunifu wa mavazi, namshukuru Mungu kwa kipaji alichonipa kinachoweza kunitambulisha na kunifanya niaminike hata kufikia hatua ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kumvalisha Rais mpya wa Zambia, Mheshimiwa Edgar Lungu”, alisema Ngowi.
 
Mbunifu Ngowi alisisitiza kuwa juhudi, nidhamu, bidii na kumweka Mungu mbele ndio chachu ya mafanikio katika kila utendaji wa kazi zake akiwa na malengo ya kuipeleka kazi yake katika nyanja za kimataifa hata kutambulika katika sekta ya ubunifu wa mavazi duniani kote.
 
Hafla hiyo ilihudhuriwa na aliyekuwa Rais wa muda wa Zambia, Guy Scott na mke wake Charlotte, Mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini(SADC), Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, baadhi ya viongozi wa juu wa Zambaia na nchi mbalimbali pamoja na wananchi wake.
 
Mbunifu huyo ameendelea kuonyesha na kudhihirisha kuwa Tanzania ni nchi yenye vipaji vinavyoweza kuiletea nchi ya Tanzania sifa na kuinua uchumi wake katika sekta mbalimbali.
 
 Hii si mara ya kwanza  kwa mbunifu huyo kukata mawingu kuitangaza nchi yetu, kwani ni miongoni mwa wabunifu mashuhuri kutoka Afrika wanaopata fursa kuonyesha ubunifu wa mavazi yao katika maonyesho ya kimataifa kama vile New York Fashion Week nchini Marekani na Mercedes Benz fashion Week nchini Afrika Kusini.
 
Hii ni changamoto pia kwa wabunifu wa Tanzania kuziwania fursa zilizopo na pia kuongeza juhudi ili kutangaza na kupeleka kazi zao katika soko la kimataifa kama vile Sheria Ngowi alivyofungua mlango.
 
 

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI