MUME NA MKE WAFARIKI DUNIA KWA KULA UYOGA



WATU wawili wa familia moja wamefariki dunia katika Kijiji cha Masyalele, Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara baada ya kula uyoga unaosadikiwa kuwa sumu. Pia wengine wanne walazwa akiwamo mtoto wa miaka mitatu katika kituo cha afya cha Mangaka.
 
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya mume na mke kufikishwa katika kituo hicho cha afya Januari 24 mwaka huu ambapo walilazwa lakini baada ya muda mfupi walifariki.
 
Akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Salvatory Chinguile alisema kuwa marehemu hao baada ya kufikishwa katika kituo hicho hawakusema ukweli kama wamekula uyoga na baada ya kufanyiwa uchunguzi walikutwa wana malaria kali.
 
“Baada ya kufika katika kituo cha afya hawakusema kama wamekula uyoga na ndipo tuliwafanyia uchunguzi na kukuta wana malaria kali na kuwaanzishia matibabu lakini walifariki wakati wakiendelea na matibabu hayo,” alisema Chinguile.
 
Dk Chinguile aliwataja marehemu hao kuwa ni Hasani Mtumbele (68) na mkewe Zena Ibrahimu (55). Waliolazwa ni pamoja na Shamila Faina (19), Mohamed Milinje (69), Maimuna Bakari (29) na Keshneti Kazumari (3).
 
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha kula uyoga ili kuepukana na madhara ambayo yanaweza kujitokeza pamoja na kusababisha vifo.
 
“Nawaomba na nashauri wananchi wote waache kula uyoga kwa sasa kwani wanaweza kupata madhara makubwa hata kusababisha vifo kutokana na uyoga mwingi kuwa na sumu,” alisema Kiswaga.
 
Pia alisema kuwa wilaya imepeleka timu ya madaktari watatu kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi wananchi wa eneo hilo ambao walikula uyoga tangu zilipoanza mvua.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA