KASHFA YA TEGETA ESCROW; VIGOGO WAWILI SERIKALINI KIZIMBANI


Watuhumiwa wa kesi ya kupokea rushwa kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrwo, Rugonzibwa Mujunangoma (kushoto) na Theophil Bakwea  na wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka. 

Miezi michache baada ya kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi, watumishi wawili waandamizi wa Serikali wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakituhumiwa kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha zilizotoka kwenye akaunti hiyo.

Mahakama hiyo ilielezwa jana kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001.
Kadhalika, Mahakama ilielezwa kuwa Februari 12, 2014, Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati na Madini, Theophillo Bwakea alipokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia akaunti yake namba 004101102643901.
“Upelelezi wa kesi umekamilika naomba mahakama izuie akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea fedha hizo za escrow na kesi ipangwe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali,” alisema Leonard Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 11 ya mwaka 2015 inayomkabili Mujunangoma, Swai alidai mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kupambana na Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007.
Swai alidai kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, Mujunangoma akiwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mujunangoma alikana na mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria anachoshtakiwa nacho, mshtakiwa huyo hahitaji kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Emilius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi ya Serikali na kwamba kila mdhamini asaini hati ya maneno ya Sh10 milioni.
Pia, Hakimu Mchauru alimtaka mdhamini ama mshtakiwa mwenyewe, kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha taslimu anazodaiwa kuzichukua kama rushwa, ama kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa masharti hayo, mshtakiwa alipata wadhamini wawili wanaoaminika , kutoa hati mbili za mali isiyohamishika ambazo alidai zina zaidi ya thamani ya fedha iliyomo ndani ya hati ya mashtaka.
Kuhusu kuzuia akaunti ya mshtakiwa, Hakimu Mchauru aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha maombi mahakamani hapo na kuyaambatanisha na hati ya kiapo itakayounga mkono maombi hayo.

Kwa upande wa Bwakea, aliyefunguliwa kesi namba 12 ya 2015, Swai alidai kuwa siku hiyo ya tukio katika benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA