FALCAO ATOROKA UWANJANI



           Radamel Falcao
MAJI ya shingo na hali si shwari. Ndivyo inavyoonekana kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia wa Manchester United, Radamel Falcao baada ya kupigwa benchi juzi na kuamua kuondoka uwanjani kwenda kutazama mechi nyumbani.
Staa huyo aliye kwa mkopo kutoka Monaco, aliachwa katika kikosi cha wachezaji18 kilichoiwakilisha United dhidi ya Southampton na kuchapwa bao 1-0 nyumbani Old Trafford.
Falcao anayelipwa Pauni 260,000 kwa wiki hakubaki uwanjani hapo na badala yake aliamua kuwasha gari lake na kuondoka zake uwanjani akitokomea kusikojulikana huku ikidhaniwa kuwa alikuwa amekwenda kutazamia mechi hiyo nyumbani baada ya kubaini kuwa hayupo katika mipango ya kocha.
Kutojumuishwa kikosini kwa Falcao kuliwashangaza wengi baada ya Kocha wa Man United, Van Gaal kukiri kwamba mshambuliaji huyo hakuwa majeruhi. Badala yake Van Gaal aliwaweka katika benchi walinzi watatu, Jonny Evans, Paddy McNair na Tyler Blackett huku katika safu ya ushambuliaji akimuweka benchi kinda James Wilson.
Falcao, ambaye ameanza mechi saba tu za Man United tangu alipojiunga kutoka Monaco, ameifungia Man United mabao mawili tu muhimu katika mechi zake tano zilizopita.
Katika mechi hizo aliipatia Man United pointi katika mechi dhidi ya Stoke City na AstonVilla, lakini sasa analazimika kupigania nafasi yake na pia kuhakikishaUnited inatoa dau la Pauni 45 milioni mwishoni mwa msimu kumchukua jumla.
Hata hivyo, Kocha Van Gaal amefafanua kwa nini alimuacha nje Falcao akidai kwamba zilikuwa sababu za kisoka zaidi na si vinginevyo.
“Inabidi uangalie mahitaji ya uchaguzi wako kwa wakati huo. Kama kocha inabidi uchukue maamuzi na inabidi uangalie mchanganyiko katika timu na pia inabidi uangalie mpango wako wa mechi,” alisema Van Gaal.
“Kwa hiyo niliamua kumuacha nje ya wachezaji 18 kwa sababu inabidi nifanye mabadiliko mfano ni Shaw na Di Maria,” aliongeza kocha huyo Mdachi.
Katika kikosi hicho United ilianza kwa kuwatumia mastaa wake wengine wote wanne katika safu ya ushambuliaji, Robin Van Persie, nahodha Wayne Rooney, Angel Di Maria na Juan Mata. Hata hivyo United ilitota kwa bao la Dusan Tadic katika dakika ya 69 ya mchezo huo.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA