PANYA ROAD 119 WAACHIWA KWA KUSOSEKANA USHAHIDI, 959 WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu  Dar es Salaam Suleiman Kova
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu  Dar es Salaam limewaachia huru vijana 119 wanaodaiwa  kujihusisha na vitendo vya kihalifu  maarufu kama ‘panya road’  baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha.
Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova amesema vijana hao walianza kukamatwa Januari 3 mwaka huu na hadi sasa wamekamatwa watuhumiwa 1,508.
Kamanda Kova amesema  watuhumiwa 119 walioachiwa huru nyendo zao zinafuatiliwa endapo watabainika wanajihusisha na uhalifu wa aina yeyote watakamatwa kwenye msako unaoendelea.
 “Mpaka sasa tumewakamata vijana 1,508 kwa tuhuma za wizi, kujeruhi, kujihusisha na dawa za kulevya, wapiga debe waliokuwa wakiwabugudhi abiria, kucheza kamari, biashara ya ukahaba na mikusanyiko isiyo ya halali katika vijiwe, tunaendelea kufanya nao mahojiano’amesema Kamanda Kova.
Amesema pamoja na watuhumiwa hao kukamatwa hadi sasa vijana 959 tayari wameshafikishwa katika mahakama mbalimbali za jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria.
Aidha Kamanda Kova amesema watuhumiwa wengine 430 wameachiwa kwa dhamana wakisubiri kukamilika kwa upelelezi huku nyendo zao zikifuatiliwa kwa ukaribu kwa kushirikiana na  wazazi wao na viongozi wa maeneo yanayowazunguka.
Kamanda Kova ametoa wito kwa raia wema kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhakika  ili makundi yanayofanya uhalifu wa aina ya panya road na mengine yaweze kutokomezwa .
“Raha ya jeshi la Polisi nchini ni kuona wananchi wa jiji la Dar es Salaam na watanzania wote kwa ujumla waishi na kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa amani na utulivu uliozoeleka, hivyo tutachukua hatua stahiki ili kukabiliana na uhalifu wowote unaoweza kuharibu amani ya nchi, amesema Kamanda Kova
Amesema jeshi hilo litaendelea kufanya msako maeneo mbali ya Dar es Salaam na mikoa mingine ili kuhakikisha matukio, ama makundi ya kihalifu yanamalizika kabisa.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI