MAZUNGUMZO YA AMANI YA SUDAN KUSINI YAANZA



         baadhi ya Viongozi walioshuhudia utiwaji saini mkataba wa aman
Harakati za kupata suluhisho la kudumu la mgogoro wa Sudan Kusini zimeanza baada ya viongozi wanaohasimiana ndani ya chama tawala cha SPLM kutia saini mazungumzo ya amani mjini Arusha jana. 
Je, makubaliano ya viongozi wa chama hicho yaliyofanyika yataweza kurejesha amani katika taifa hilo changa kuliko yote duniani? Salva Rweyemamu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Tanzania, anasema utengamano ndani ya chama cha SPLM kutaleta amani ndani ya Sudan Kusini.
"katika Sudan Kusini chama kikuu cha siasa ni SPLM. Siasa zote za Sudan Kusini zinafanyika katika chama hicho.Kwa hiyo yanapotokea makubaliano yanayojaribu kukiunganisha upya na kukileta pamoja upya chama cha SPLM, maana ni hatua kubwa, hatua ya kihistoria, hatua ambayo kwa namna fulani inatuweka mahali ambapo sasa, tunaweza kutafuta suluhisho la amani ya kudumu Sudan Kusini" amesema Salva.
Utulivu ndani ya chama tawala cha SPLM utaharakisha mazungumzo ya kutafuta amani nchini Sudan Kusini kupitia mazungumzo ya amani yanayofanyika Addis Ababa, yanayosimamiwa na nchi za IGAD. Bwana Salva anasema mazungumzo ya Arusha hayatengui mazungumzo yanayofanyika Addis Ababa. "kilichofanyika Arusha ni kutia saini makubaliano ndani ya chama chenyewe, kusudi tuanze sasa kutafuta suluhisho ndani ya chama. Lakini mazungumzo ya kuleta amani yanaendelea, Addis Ababa pale, chini ya IGAD, kwa hiyo makundi mengine yote yako Addis Ababa, kwa hiyo kimsingi, hakuna mtu atakayeachwa nje katika mazungumzo haya, na kwa kweli ukiacha watu nje ndio unaendeleza uhasama.
Viongozi mbalimbali wameunga mkono makubaliano ya Arusha yaliyosimamiwa na chama tawala nchini Tanzania, CCM katika kuwapatanisha viongozi wa chama tawala na rafiki cha Sudan Kusini, SPLM.
Shughuli ya kutia saini mazungumzo hayo kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa naibu wake Riek Machar zilishuhudiwa na viongozi mbalimbali, miongoni mwao ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na naibu rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na maafisa wengine kutoka Umoja wa Afrika.
Mgogoro wa Sudan Kusini umesababisha vifo vya watu zaidi ya 10,000, huku watu zaidi ya milioni moja kukosa makazi na kuisukuma nchi hiyo kuelekea katika baa la njaa.Umoja wa Ulaya na Marekani zimewawekea vikwazo makamanda kutoka pande zote mbili za mgogoro, kwa kukiuka mapatano ya kusitisha mapigano.
Mapigano yamekuwa yakiongezeka kwa misingi ya ukabila, huku majeshi yanyomtii Kiir, kutoka kabila la Dinka, wakipambana na wafuasi wa Machar, wa kabila la Nuer. Machar alifukuzwa kuwa naibu rais mwezi Julai na kuongeza upinzani wao uliodumu kwa miaka mingi.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA