UWASILISHWAJI WA RIPORT YA PAC KUHUSU TEGETA ESCROW ACCOUNT



Baada ya bunge kwenye kikao cha asubuhi kusema swala la Escrow limeingizwa kwenye ratiba na ripoti itawasilishwa kuanzia jioni ya leoTujumuike kwa pamoja kuhabarishana yanayojiri jioni hii bungeni Dodoma kuhusu sakata la Escrow.

Anaekalia kiti jioni hii ni spika mwenyewe mama Anna Makinda

Katibu: Bunge lipokee na kujadili ripoti maalumu

Waziri wa sheria(Migiro): Katiba ya jamuhuri imezingatia mgawanyo wa mihimili, kuna zuio la muda la mahakama, shauri hili la 2014 lilikua na nia bunge lisijadili ripoti, mahakama katika barua yake ilikusudia bunge liendelee shughuliki zake kama zilivyopangwa.

Makinda: Spika anatoa nasaha chache kabla hajaruhusu mjadala na Zitto anaitwa

ZITTO: Taarifa ina sehemu mbili na itasomwa na mwenyekiti na makamu mwenyekiti na anaanza kuisoma ripoti, Migogoro ilitakiwa iishe kwanza ili pesa zililipwe 2014 March kamati ya PAC ilikutana na BoT ili kujadili pesa zilizo kwenye walisema pesa zimeshatolewa na zimeshalipwa IPTL, kamati iliomba ofisi ya CAG kufanya ukaguzi.

Majadiliano bungeni: Waheshimiwa wabunge wamejadiliana kwa namna tofauti, kundi la kwanza wamekuwa wakisema fedha hizo ni za umma na kundi la pili wamekuwa wakisema ni fedha za IPTL na zilikuwa sawa kulipwa IPTL.

Anawataja wanakamati waliochambua waliochambua ripoti, kwanza kamati ilifanya uchambuzi wa mkataba wa kufua umeme. Serikali 1995 iliingia mkataba wa kuuziana umeme kwa miaka 20 lakini mkataba wa awali ni miaka 15


Mwaka 1997 ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ulikamilika. Hata hivyo, TANESCO ilibaini kwamba gharama za ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme ambazo IPTL iliwasilisha kwake zilikuwa kubwa tofauti na makubaliano ya kwenye Mkataba. IPTL ilikuwa imefunga injini zenye msukumo wa kati ( medium speed) zenye gharama ndogo na uwezo mdogo badala ya injini za msukumo mdogo ( low speed) zenye nguvu kubwa na bei kubwa. Wakati huo huo IPTL waliendelea kutoza kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na gharama ya ufungaji wa mtambo wenye msukumo mdogo ( low speed) .

Kutokana na IPTL kukiuka makubaliano ya Mkataba kama ilivyoelezwa hapo juu, mwaka 1998 TANESCO ilifungua Shauri Na. ARB/98/8 katika Baraza la Kimataifa la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (The International Centre for Settlement of Investiment Disputes - ICSID) kupinga ukiukwaji huo. Katika Hukumu iliyotolewa na ICSID, IPTL iliagizwa kupunguza gharama za uwekezaji kutoka USD 163.531 milioni hadi USD 127. 201 milioni kwa mwezi.

Ujenzi wa Mtambo ulikamilika mwaka 1997 lakini uzalishaji na uuzaji wa umeme ulianza mwaka 2002. Kwa mujibu wa makubaliano ya kuzalisha umeme, TANESCO ina wajibu wa kulipia gharama za uwekezaji ( capacity charges ) kwa wastani wa USD 2.6 milioni kila mwezi.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imebainika kuwa chanzo cha mgogoro kati ya TANESCO na IPTL ambacho ndio kilisababisha kufunguliwa kwa Akaunti ya Tegeta ESCROW, ni taarifa ziliyoifikia Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO mnamo tarehe 01 Aprili, 2004. Kaika Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine walifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, Kampuni ya VIP Engineering, kuwa kuna viashiria kuwa TANESCO wanailipa IPTL capacity charges kubwa.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO iliiteua Kampuni ya Uwakili ya Mkono ili kufuatilia madai hayo na kutoa ushauri kwa Bodi

Kwa kuzingatia ushauri wa Kampuni ya Uwakili ya Mkono, Menejimenti ya TANESCO kupitia barua namba DMDF&CS/02/05, tarehe 17 Juni, 2004 walitoa Notisi kwa IPTL ya kutoendelea walichokuwa kulipa capacity charges kwa sababu kiwango wanatozwa ni kikubwa kuliko inavyostahili.

Pamoja na kutoa Notisi hii Kamati imebaini kuwa Bodi na Menejimenti ya TANESCO kwa nyakati tofauti walizitaarifu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Nishati na Madini, na Msajili wa Hazina kuomba zichukue hatua stahiki kutatua mgogoro uliokuwa unaendelea. Kamati ilifanikiwa kuona barua Na. NEM/740/05 ya tarehe 6 Desemba, 2005 kutoka kwa Kampuni ya Uwakili ya Mkono kwenda kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. Patrick Rutabanzibwa akirejea mazungumzo yao ya tarehe 5 Desemba, 2005 ambapo iliamuliwa kuwa Kampuni ya Uwakili ya Mkono iandae Rasimu ya Makubaliano kwa ajili ya ufunguzi wa Akaunti ya Tegeta ESCROW.

Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 
“... Kwa jinsi tulivyopitia fedha hii, tungesema ipo katika makundi matatu. Kundi la kwanza hiyo fedha ilikuwa na kodi ndani yake kwa hiyo tungesema kulikuwemo na fedha ya Serikali kwa maana ya kodi. Kwa upande mwingine, kwa sababu mpaka ESCROW inafunguliwa kulikuwa na dispute, kulikuwa na kutokubaliana juu ya charges, kwa hiyo kuna fedha ambayo inaweza ikawa ni ya TANESCO na kuna fedha ambayo inaweza kuwa ni ya IPTL ...”

Kamishna Mkuu wa TRA
“... TANESCO walitudhihirishia na kwa evidence kwamba katika kufanya yale malipo kwenye ESCROW Account walilipa pamoja na pesa ambayo ilitakiwa kulipwa kwetu ya VAT. Kwa hiyo, kulikuwa na VAT Component ambayo haikutakiwa kwenda kule ... 


Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
“... fedha za ESCROW hizi ni fedha zilizowekwa baada ya hawa wafanyabiashara wawili kutokukubaliana na zingeweza kuwekwa popote ... kwa hiyo hizo pesa ni za IPTL, yaani ni kitu ambacho ni rahisi kabisa, lakini mtu anataka kupotosha hapa anasema fedha za walipa kodi, fedha sijui za wakulima, hakuna kitu kama hicho

MAUZO YA HISA ZA IPTL
Umiliki wa hisa unakamilika pale ambapo muuzaji anamkabidhi mnunuzi Hati ya hisa husika, vinginevyo mnunuzi anakuwa amenunua “hisa hewa”. Pamoja na ukweli huu bado Piper Links tarehe 21 Oktoba, 2011 ilimuuzia PAP hisa zile saba kwa gharama ya USD 20 milioni. Swali linalojitokeza hapa ni kuwa unawezaje kuuza kitu usichonacho?

Kutokana na mahojiano kati ya Kamati na Kamishina Mkuu wa TRA ilibainika kwamba Kampuni ya Piper Links haijulikani sio tu British Virgin Islands bali hata nchi nyingine. 20 Kamati haielewi ni jinsi gani taasisi kubwa kama Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na nyingine zilizohusika katika suala hili, na ambazo tunaamini zimesheheni Watendaji wenye weledi, zimewezaje kushindwa kufanya uchunguzi wa kina ( due diligence ) ambao ungewezesha utata huu kugundulika na kuepuka kudanganywa na PAP.

Hisa kutoka Piper Links kwenda PAP ziliuzwa kwa gharama ya USD milioni 20, lakini taarifa zilizopelekwa TRA zilionyesha kuwa hisa hizo zimeuzwa kwa USD 300,000. Kwa mantiki hiyo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Piper Links ilitozwa na kulipa kodi ya ongezeko la mtaji kiasi cha Sh. 47,940,000 na Sh. 4,800,000 kama ushuru wa stempu ( stamp duty) ’. Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa TRA aliifahamisha Kamati kuwa kwa gharama ya USD milioni 20 kiasi cha kodi ya ongezeko la mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh. 6,399,977,600 na sio Sh. 47,988,800, na kwa upande wa ushuru wa stempu ‘stamp duty’ kiasi kilichotakiwa kulipwa ni Sh. 320,000,000 na siyo Sh. 4,800,000. Kwa maana hiyo jumla ya kodi iliyopotea kwa maana ya kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ( stamp duty) ’ ni Sh. 6,667,188,800.

Jumla ya kodi iliyopotea kutokana na uuzaji wa hisa za Mechmar kwenda Piper Links na za Piper Links kwenda PAP ni jumla ya shilingi 8,683,177,600.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA