SIMBA YAANZA USAJILI


          Kikosi cha Simba FC


ZIMEBAKI siku 61 kuanzia leo Jumamosi kuumaliza mwaka 2014 na kuingia mwaka 2015.
Simba ambayo bado haijapata matokeo mazuri hadi sasa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, imeanza mikakati mipya miwili ambayo lazima ikamilike kabla jua la 2014 halijazama.
Mpango wa kwanza ni kushinda mechi zote tatu za ligi zilizobaki mwaka huu wakianza na ile dhidi ya Mtibwa Sugar inayochezwa leo Jumamosi mjini Morogoro, kisha za Ruvu Shooting na Kagera Sugar.
 Jambo la pili ambalo ndilo mashabiki wa Mnyama wangependa kulisikia zaidi ni kwamba viongozi wameanza mchakato wa usajili mpya wa dirisha dogo.
Simba imeanza mazungumzo ya awali na mshambuliaji matata wa Mtibwa Sugar, Ame Ally, ambaye ni ni Mzanzibari na imeelezwa kwamba ipo tayari kuzama benki kuchota noti za maana kumshusha Msimbazi mchezaji huyo pamoja na wengine ambao tayari kazi ya kuwanasa inaendelea kimya kimya. Ame ana mabao mawili kwenye Ligi Kuu Bara mpaka sasa kama ilivyo kwa Shaban Kisiga (Simba), Agrrey Morris (Azam), Emmanuel Okwi (Simba) na Jabir Aziz (JKT Ruvu)
Kamati ya Usajili ya Simba inayoongozwa na Mwenyekiti, Zacharia Hans Poppe na Makamu wake, Kasim Dewji ‘KD’, imepanga kufanya mabadiliko ndani ya kipindi kifupi cha dirisha dogo litakaloanza Novemba 15 mpaka Desemba 15 ili kuifufua Simba tayari kwa vita ya mwakani.
Kocha Patrick Phiri aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa hataki kuwa na wachezaji wengi wapya kwani itakuwa ni kama kuanza kuijenga Simba upya, aliowakuta wengi wao ni wapya hivyo alipendekeza kuimarisha zaidi safu ya kipa, straika, kiungo mkabaji, beki ya kati, beki ya kulia na kushoto, ambapo anahitaji mchezaji mmoja mmoja kila safu.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba wachezaji zaidi ya watano watatemwa katika dirisha hilo dogo. Wanaotajwa kutemwa ni  kipa Ivo Mapunda, Amri Kiemba, Haroun Chanongo, Amissi Tambwe, Pierre Kwizera, Uhuru Seleman na Nasoro Masoud ‘Chollo’.
Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti kuwa awali viongozi wa Simba walikataa kumsajili mchezaji huyo wa Mtibwa kwa madai kuwa hana kiwango na hawajawahi kumwona huku wakizungumzia pia suala la umri kwamba ni mkubwa. Ame ameifungia timu yake mabao mawili na ameonyesha kiwango kizuri tangu kuanza kwa msimu huu.
“Kabla hajaenda Mtibwa mchezaji huyo alikuja Simba lakini walimkataa, hivyo akaona ni vyema aende Mtibwa ambako walimhitaji lakini cha ajabu sasa hivi wanaanza kumtamani tena na kuanza kumfukuzia ambapo tayari ana mkataba na Mtibwa Sugar, hawakutana kumwona hata mazoezini. Kinachofanyika sasa ni kumalizana na Mtibwa na Mchezaji husika ambayo si gharama kubwa,”alidokeza kiongozi huyo.
Mbali na mshambuliaji huyo, imeelezwa kwamba kipa wa Yanga Juma Kaseja ni miongoni mwa makipa wanaowaniwa na Simba kwa kile kilichoelezwa kuwa kutemwa kwa Ivo kunabakiza makipa wawili Hussein Sharif ‘Casillas’ ambaye ni majeruhi na Manyika Peter ambaye usajili wake ni wa U-20 na pia kuna taarifa za Kaseja kuomba kuvunja mkataba wake na Yanga kwa vile hatumiki na hajalipwa stahiki zake.
Wakati Simba inahaha kutafuta vifaa vipya wenzao Yanga hawana papara kwani hawatahitaji marekebisho makubwa.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA