TAMBWE AIKARIBIA YANGA



              Ammis Tambwe
MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Amissi Tambwe, kwa sasa anaonekana si lolote katika timu yake ya Simba ambapo amefunga bao moja tangu msimu huu uanze, lakini imebainika kuwa mfumo anaotumia kocha wao Patrick Phiri ndio chanzo cha kuporomoka kwa straika huyo.
Mchezaji huyo ambaye ameanza kuwatamanisha baadhi ya viongozi wa usajili wa Yanga, ametamka kwamba anamalizia mechi zake mbili zilizobaki Simba kufunga mwaka halafu arudi kwao Burundi ambako anaweza kufanya uamuzi mgumu kutokana na vitisho alivyopata klabuni kwake hivi karibuni.
Habari za ndani zinadai Tambwe ambaye amebakiza miezi mitano katika mkataba wake ameanza kujadiliwa na baadhi ya vigogo wa Yanga ambayo tayari ina wachezaji watano wa kigeni, lakini mtihani ni jinsi ya kumshawishi kocha Mbrazili Marcio Maximo.
Hata hivyo mabosi hao wanadai watajua cha kufanya baada ya kumaliza mechi zilizosalia mwaka huu na kusikia tathmini ya Kocha. Wakati Simba ilipokuwa chini ya kocha, Zdravko Logarusic, kocha huyo alikuwa hampi majukumu mengi Tambwe huku kazi yake kubwa ikiwa ni kukaa eneo moja na kusubiri mipira ya kufunga ambapo alikuwa kitumia mifumo ya straika mmoja mbele 4-5-1 au 4-2-3-1.
Lakini Phiri amempa Tambwe majukumu mawili ambapo anashuka kutafuta mipira na kupanda kufunga jambo ambalo limekuwa gumu kwake kumudu majukumu mawili kwa wakati mmoja. Phiri hupendelea sana kutumia mifumo ya 4-4-2, 4-3-3 na 3-5-2.
Tambwe alikiri kuwa mabadiliko hayo pia yamechangia kiwango chake kuonekana kushuka kwani hawezi kufanya yote hayo kwa wakati mmoja. “Kila kocha ana mfumo wake wa ufundishaji, nilipokuwa chini ya Loga sikuwa na majukumu mengi katika timu, lakini hivi ninapewa majukumu mengi ambayo si rahisi kuyafanya kwa wakati mmoja na kuleta mafanikio, hivyo nalazimika kucheza kutokana na kocha anavyotaka,” alisema Tambwe.
Tambwe pia ni miongoni mwa wachezaji wanaotuhumiwa kucheza chini ya kiwango kutokana na matokeo ya sare tano mfululizo huku akitajwa kuwa ni mmoja wa wachezaji watakaotemwa kwa kosa hilo ambapo yeye amesema kwamba yupo tayari kuondoka ili kupisha wengine watakaoisaidia Simba.
“Nipo katika wakati mgumu sana kwa sasa, tuhuma zimezidi jambo ambalo si kweli, nakosa amani ndani ya timu hivyo sioni sababu ya kuendelea kuwepo sehemu ambayo maisha yangu yapo hatarini, maisha ya mpira ndivyo yalivyo lakini kwa sasa yamezidi maana imefikia hatua natumiwa ujumbe wa vitisho, sasa nasubiri nini Simba? Nataka nikapumzike kidogo,” alisema Tambwe
Tambwe pia alikuwa mfungaji bora katika michuano ya Kombe la Kagame alipokuwa na timu yake ya Vital’O ya Burundi 2013 yaliyofanyika Sudani Kusini ambapo alifunga mabao sita.
Lakini Phiri, alisema hupenda kutumia mifumo hiyo ili timu iweze kushambulia zaidi na kupata mabao, pia alikiri wachezaji wengi wameathirika kisaikolojia kutokana na matokeo wanayoyapata.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA