KELELE ZAWAKIMBIZA OKWI, JAJA DAR

KITENDO cha Yanga na Simba kushindwa kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara tangu msimu huu uanze, kimewaweka mastraika wawili kwenye presha kubwa na timu zao zimeondoka kwenye ardhi ya Dar es Salaam zikiwa na kiu kali  ya kusaka ushindi ugenini kwenye mechi mbili ngumu.
Mafowadi hao waliotwishwa mzigo mkubwa wa ushindi na mashabiki ni Genilson Santos ‘Jaja’ wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba.  Wawili hao watakuwa tegemeo kubwa kwa timu zao ndani ya siku 14 watakazokuwa mikoani na endapo ushindi usipopatikana kwa nguvu zao au kupitia wachezaji wengine, huenda hali ya hewa ikabadilika kwenye klabu zao kutokana na mwenendo usiovutia kwenye timu hizo kongwe za soka nchini. 
Baada kutoka suluhu na Simba, Kocha wa Yanga, Marcio Maximo, alisema nguvu zao zote wanazihamishia mikoani ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi wakati Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri yeye amesema iwe isiwe ni lazima timu yake ipate ushindi mikoani.
Simba ambayo ndiyo timu pekee kwenye ligi hiyo ambayo haijashinda mchezo wowote mpaka sasa kama ilivyo Polisi Moro, itasafiri kwenda mkoani Mbeya kucheza na Prisons wikiendi hii na kisha itahamia Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya pili ili kukamilisha siku zao 14 nje ya Dar es Salaam.
Yanga ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo nyuma ya Azam, Mtibwa na Coastal Union, itasafiri kwenye  Shinyanga kucheza na Stand United, kisha itaelekea Kagera kucheza na Kagera Sugar ili kukamilisha siku hizo 14 ambazo Maximo anaziita siku za hatari na kisha kurejea Dar es Salaam.
Simba ikiwa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo, inakwenda mikoani ikiwa na kumbukumbu ya kucheza mechi nne Dar es Salaam bila kupata ushindi wowote, ikiwa imetoka sare mara nne na kufikisha pointi nne wakati Yanga wao  tayari wamecheza mechi moja nje ya Dar na kupokea kipigo cha mabao 2-0  kutoka kwa Mtibwa kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi kabla ya kuzifunga Prisons na JKT Ruvu mabao 2-1 kila moja na kutoka suluhu na Simba.
Phiri alisema: “Nafahamu kuwa viwanja vya ugenini ni vigumu kucheza, lakini tunatakiwa kushinda, mechi hizo mbili ni changamoto, lakini tutapambana ili tuweze kushinda zote pamoja na ile ya tatu tukayocheza kabla ya ligi kusimama.
“Naandaa aina ya wachezaji wanaoweza kutusaidia mikoani kama Elius Maguli, hao ni wachezaji wenye uwezo wa kupambana na wamevizoea viwanja hivyo.”
Phiri alikiri kuwa kuna baadhi ya wachezaji wa kikosi chake ambao wamecheza vizuri mechi za Dar, lakini hawana uwezo wa kucheza mechi za mikoani.
Kwa upande wake, Maximo anayesifika kwa kuwa na msimamo mkali alisema:  “Sare na Simba kwa sasa ni historia, tunaelekeza nguvu zetu zote kwenye mechi ya Stand United ili tuweze kupata pointi zote tatu na kujiweka pazuri kwenye msimamo.

“Najua haitakuwa kazi rahisi kwani Stand ni timu nzuri na imejipanga vizuri,   hata mechi zao wamecheza kwa kiwango cha juu, ni dhahiri kuwa tutakuwa na kazi ngumu.”
Simba itakwenda kucheza na Prisons ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare moja na kushinda mara moja katika mechi zake mbili za mwisho ilizocheza na timu hiyo kwenye Uwanja wa Sokoine.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA