PAZI AKAMILISHA MPANGO WA KASEJA KUTUA SIMBA


             
                                            Juma Kaseja

KOCHA wa zamani wa Makipa wa Simba, Idd Pazi, amesema sasa ni muda mwafaka kwa kipa, Juma Kaseja, kurejea kwenye kikosi cha klabu yake hiyo ya zamani kutokana na uzoefu mkubwa alionao.
Hivi karibuni kumekuwapo na taarifa za Kaseja kurejeshwa kwenye kikosi cha Simba ili akasaidiane na kipa chipukizi, Peter Manyika Jr pamoja na Hussein Shariff ‘Casillas’ kwani Ivo Mapunda anahusishwa na mpango wa kutemwa kikosini hapo.
Pazi ambaye hivi karibuni aliondolewa kuinoa Simba baada ya klabu hiyo kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, alisema Kaseja anaweza kuisaidia klabu hiyo lakini ameutaka uongozi wa kutatua matatizo mengine yanayochangia klabu hiyo kufanya vibaya.
“Kaseja ni kipa mzoefu, ataisaidia Simba hivyo siyo jambo baya kumrejesha, pia amekuwa na historia nzuri na klabu hiyo kwa muda wa miaka 10 aliyokuwa pale,” alisema.
“Hii pia itamsaidia Manyika ambaye ndiyo kwanza anakua, kuna mechi ambazo anaweza kudaka lakini nyingine ni lazima adake kipa mwenye uzoefu.”
Akizungumzia matokeo mabaya yanayoikabili Simba kwa sasa, Pazi alisema viongozi wanafahamu kiini cha tatizo, lakini wamegoma kuyatafutia ufumbuzi jambo linaloendelea kuigharimu timu.
“Kuna mambo ya nje ya uwanja ambayo yanachangia timu kuboronga, viongozi wanayafahamu lakini ni kama wameyafumbia macho, wajitahidi kuyatafutia ufumbuzi ndipo wawaze kufanya usajili,” alisema Pazi.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA