AKIMBIWA NA MKE BAADA YA MGUU WAKE KUOZA

“NAJUTA kuzaliwa, sikujua kama maisha yangu yangebadilika kuwa katika hali hii! Mke amenikimbia, jamii imenitenga, sina rafiki, ndugu nao hawanipendi. Haya yote yananikuta kwa sababu ya huu ugonjwa ambao sikuuomba,” ndivyo alivyoanza kusema huku akilia, Seleman Juma (pichani).
Seleman mwenye miaka 38 na mkazi wa Vingunguti jijini Dar amekimbiwa na familia yake kutokana na ugonjwa wa Matende unaomsumbua na amejikuta akiishi peke yake katika mazingira yasiyostahili binadamu kuishi.
 HISTORIA FUPI YA MAISHA YAKE 
“Mimi ni mtoto wa tatu kati ya wanne, katika familia yetu. Tulizaliwa Kijiji cha Masimba wilayani Kisarawe, Pwani, nimebaki na mama baada ya baba kufariki dunia mwaka 2010.
“Sina elimu yoyote, kwani sijawahi kwenda shule hata chekechea, naamini wazazi wangu walichangia.
 “Mwaka 1997, kutokana na ugumu wa maisha niliamua kuja jijini Dar kutafuta, nikawa nafanya kibarua katika Machinjio ya Vingunguti

“Mwaka 1999 nilimuoa Aisha Salum. Mwaka 2002 akajifungua mtoto wetu wa kwanza, tukampa jina la Sikujua. Kwa bahati mbaya alifariki dunia. Hapa naomba ieleweke kwamba mpaka wakati huo sikuwa na tatizo hili la mguu.
 “Mwaka 2005 Mungu akatupa mtoto mwingine, tukampa jina la Mwajuma. Wakati huo nilikuwa naendelea na shuguli zangu za machinjioni na nilikuwa nikiishi kwa mapenzi makubwa na familia yangu  kule Vingunguti.
 TATIZO LAANZA
“Mwaka 2008 katika hali ambayo sikuitarajia, mguu wangu wa kulia ulianza kuuma na kuvimba. Nilishangaa ingawa si kwa kiwango cha kufikiria hali hii, baadaye kwenye uvimbe kulipasuka na kutoa usaha mwingi na harufu kali.
 “Niliamua kwenda Hospitali ya Amana kisha Muhimbili bila mafanikio, madaktari waliniambia huenda nilikuwa na tatizo la tende. Mguu uliendelea kutoa harufu kali sana, hata mimi nilitamani usiwe wangu.
 WAPANGAJI WAMTENGA, WAOMBA AFUKUZWE
“Niliumia zaidi baada ya kubaini kwamba wapangaji wenzangu walianza kumlalamikia mwenye nyumba na kutishia kuhama kama hatanifukuza mimi,” Seleman alianza kulia hapo akidai kuwa akikumbuka anaumia sana.
“Mwenye nyumba ingawa alikuwa ananipenda lakini ilimbidi aniambie ukweli kwamba  nitafute pa kuelekea.
 “Siku ananiambia zilibaki siku tatu kodi ya nyumba iishe, kwa hakika hakuna aliyenipenda kutokana na harufu ya huu mguu. Kuna wakati hata mke wangu alikuwa akinichukia.
“Ni binti yangu pekee ndiye aliyekuwa akinipenda, mke wangu alifika mahali akawa hataki tulale kitanda kimoja, alinishusha chini akidai nanuka. Ilibidi nifanye hivyo.
 MKE AINGIA MITINI
“Siku moja mke wangu akaniambia kuwa amepata chumba kule Yombo, akashauri tukaishi huko. Mimi nilikuwa nina watu nawadai kama shilingi laki tatu (300,000/-), nilitafuta pikipiki ili kwenda kudai fedha hizo ili nimpe mke wangu akalipie hicho chumba.
 “Niliporudi jioni sikumkuta, alichukua kila kitu kisha akatoweka na mwanangu. Niliumia sana na nilichanganyikiwa. Nilimpigia simu na kumuuliza nini kilimpata, akaniambia mkataba wa kuishi na mimi uliishia pale, akakata simu na kuanzia hapo ikawa hapatikani tena.
 AMFUATA MDOGO WAKE LAKINI NAKO...
“Niliondoka kwenda kwa mdogo wangu hapahapa Vingunguti, nilikuta begi langu na baadhi ya nguo. Ina maana kwamba mke wangu alipotoka nyumbani aliamua kupeleka mizigo yangu kwa huyo mdogo wangu. Sawa lakini, Mungu yupo na dunia ni hiihii tu hakuna nyingine.
 “Basi, mdogo wangu alinionea huruma sana, akaniambia niendelee kuishi naye wala nisiwe na wasiwasi. Nilifarijika kwa kauli yake hiyo, niliishi pale kwa muda wa miezi miwili, mguu nao ukazidi kuwa mbaya, harufu ikawa inazidi.
“Pale kwa mdogo wangu napo likazuka balaa tena! Wapangaji wenzake walikuja juu, walitishia kuhama kama sitaondoka.
 Mwenye nyumba akaniambia nitafute pa kwenda kwa sababu nataka kumfukuzia wapangaji wake. Ilibidi nimwambie mdogo wangu, naye akaenda kwa mwenye nyumba kumwomba niendelee kuishi.
 MWENYE NYUMBA AMTIMUA
“Hata hivyo, mwenye nyumba alikataa katakata na kumwambia mdogo wangu kama anashindwa kunifukuza tuhame wote. Ilinibidi niondoke ili kuepuka mengi, sikujua pa kwenda, sikuwa na fedha hata ya kupangishia chumba.
“Akili ya harakaharaka iliniambia niende machinjioni nilikokuwa nafanyia kazi, nikawa nalala nje, niliofanya nao kazi walinionea huruma lakini kutokana na hali yangu ya kutoa harufu hakuna aliyekuwa tayari kunipeleka kwake.
 “Lakini nawashukuru kwani walikuwa wakininunulia chakula na kunipa fedha kidogo kwa ajili ya kulipia bafu nioge. Lakini hapo kwenye bafu napo ikawa balaa, baadhi ya wateja walikuwa hawataki nioge pale wakidai harufu ni kali na kwamba nitawaambukiza ugonjwa wangu.
 YALIPO MAISHA YAKE
“Kwa sasa bado naishi hapahapa machinjioni,  kuna ndoo nimepewa, nanunua maji kisha naoga nje usiku. Kwa sasa hali yangu imezidi kuwa mbaya, ndugu na marafiki wanazidi kunipotea, harufu inazidi, mvua ikinyesha nikijikinga upenuni mwa nyumba za watu, wananifukuza wakidai kwamba harufu inaingia ndani.
 “Kuna siku nilipata chumba, nikawa nalala sakafuni kwani mke wangu aliondoka na kila kitu, lakini pamoja na kulipa kodi ya chumba, muda ulipoisha  mwenye nyumba alinirudishia fedha zingine na kunitaka nitafute pa kwenda kutokana na kero ya harufu.
 “Sasa sina pa kwenda, niko hapahapa machinjioni katika shida ya mbu na mvua. Nikisema niende hospitali kwenye daladala, makonda wananizuia kupanda kwa vile nanuka eti nitawafukuzia abiria. Hospitali siku zile waliniambia ugonjwa wangu unaweza kutibika nchini India, sina uwezo wa kwenda huko, Watanzania naombeni msaada wenu nikatibiwe.
 ANACHOOMBA
“Akijitokeza msamaria mwema akanipa shilingi laki nne (400,000) nikapange chumba cha kuishi nitamshukuru sana.
“Pia naomba nguo, chakula na kama kuna uwezekano nisaidiwe kujengewa hata vyumba viwili kwa vile nina kiwanja huko Chanika.
 Kwa yeyote aliyeguswa na mateso ya Mtanzania huyu anaweza kumsaidia kwa kupitia namba yake ya simu 0713 746572 au kupitia kwa mwandishi wa habari hii, 0768 454656 au 0783 454656.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA