WALIOMUIBA MTOTO PENDO MWENYE ULEMAVU WA NGOZI WAKAMATWA MWANZA



Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema watu wote waliohusika ‘kuiba’ mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Pendo Emmanuel (4) katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba, Mwanza, wamekamatwa.

Akizungumza wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya wa mkoa huo jana, Manju Msambya (Misungwi), Zainab Rajab (Sengerema) na Pili Moshi (Kwimba), Mulongo alisema watu wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa bado hawafahamu kama mtoto huyo yupo hai ama mfu.
  
“Wezi wale baada ya kumuiba mtoto Pendo walimleta katika hoteli moja hapa jijini Mwanza, kisha kuwakabidhi watu walionekana wanunuzi, lakini wote hao wamekamatwa akiwamo mmiliki wa hoteli hiyo,” alisema Mulongo.
  
Alisema serikali ipo kazini wakati wote, ndiyo maana inafanya kazi usiku na mchana kuwasaka watu wote waovu mkoani Mwanza ambao hawawezi kusalimika kwa kile watakachokifanya.
  
Hata hivyo, alisema watu hao waliofanya uhalifu huo akiwamo baba wa mtoto huyo, Emmanuel Shilinde, wanashikiliwa na polisi huku mtu wa mwisho aliyetoweka na mtoto huyo toka hotelini hapo akiendelea kutafutwa.
  
Mulongo hata hivyo hakuweza kuitaja hotel wala mmiliki wake na wangine waliohusika na tukio hilo lilitokea Desemba 27 mwaka jana, lakini Shilinde akituhumiwa kuhusika zaidi na tukio hilo kutokana na kuamua kufanya hivyo kwa sababu alikuwa ana watoto wawili albino.
  
Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wakuu wa wilaya wapya, kuhakikisha kushughulikia changamoto za wapiga ramli, kuangalia utoaji wa vibali kwa waganga wa jadi ili kudhibiti matukio ya utekaji na mauaji ya albino.
  
Hata hivyo, alishangazwa na maneno yanayotolewa na watu kuhusiana na mauaji hayo kuwa yanatokana na masuala ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.
  
Katibu wa chama cha maalbino mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju, aliishutumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua stahili tangu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yalipoanza miaka tisa iliyopita.
  
Amesema kwa miaka tisa serikali inahangaika na kudai inachukua hatua lakini hakuna hatua yoyote inayoonekana mpaka sasa huku albino wengi wakiwa wanaishi vijijini katika nyumba zisizo na ulinzi thabiti, lakini utakuta viongozi wa serikali wanaenda huko pale linapotokea tatizo la mauaji ya watu hao.
  
Tuju amewashambulia mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Antony Diallo, naibu waziri wa nishati na madini, Charles Kitwanga na mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu, kwa kushindwa kufanya juhudi zozote za kuwalinda na kuwatetea albino.
  
Katika kipindi cha miezi miwili, watoto Pendo Emmanuel wa Kwimba na Yohana Bahati (mwaka mmoja) wa kijiji cha Ilelema Chato, walitekwa na watu wasiojulikana.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI