MWAKALEBELA: HAITAKUWA AJABU KUUACHA UKUU WA WILAYA


MKUU wa Wilaya mteule wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Frederick Mwakalebela amesema iwapo ushawishi na dhamira vitamtuma kuwania tena ubunge Iringa Mjini, halitakuwa jambo la ajabu kufanya hivyo, licha ya madaraka aliyopewa.
 
Ingawa amesema, sasa macho yake anayaelekeza katika kutekeleza majukumu mapya aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete katika Wilaya ya Wanging’ombe, historia inaonesha wapo wakuu wa wilaya na mikoa na viongozi wakubwa serikalini, walioamua kuacha majukumu waliyonayo na kuwania ubunge.
 
Alisema hayo juzi alipoapishwa kuwa Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Manispaa ya Iringa, ikiwa ni miezi minane kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
 
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde kwa niaba ya Naibu Katibu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba ndiye alimwapisha Mwakalebela kushika wadhifa huo.
 
Mwakalebela amekuwa akitajwa kuwa atawania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini katika uchaguzi wa mwaka huu.
 
Hata hivyo, alipoulizwa alisema muda haujafika. Mwakalebela alisema,“muda bado haujafika, nawaomba wana Iringa na wapenzi wangu wa kisiasa wawe wavumilivu, najua wananchi wengi wana shauku ya kuona jimbo hili linarejea CCM.”
 
Pamoja na kusisitiza kwamba amejielekeza kwenye majukumu ya ukuu wa wilaya, alisema, “Lakini jukumu langu la pili kama Kamanda wa UVCCM, litakuwa ni kuwaunganisha vijana ndani na nje ya CCM ili kwa pamoja tuweze kulirejesha jimbo letu la Iringa Mjini mikononi wa CCM.”
 
Jimbo la Iringa Mjini linaongozwa na Mchungaji Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Mchungaji Msigwa alishinda katika jimbo hilo kwa kile ambacho kimekuwa kikielezwa mara kwa mara na viongozi na wana CCM, kwamba ni baada ya kumuengua Mwakalebela, aliyeshinda kura za maoni.
 
Inadaiwa baada ya vikao vya chama kumsimamisha mshindi wa pili, Monica Mbega, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na mwaka huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, baadhi ya wanachama walichukizwa na uamuzi huo, jambo lililochangia kutomchagua Mbega hatimaye kumchagua wa Msigwa wa Chadema.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI