MAGUFULI AMLILIA MTOTO ALIYETEKWA NA KUUAWA, ACHANGIA SHILINGI MILIONI MOJA



WAZIRI wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa Chato, Dk John Pombe Magufuli amelaani vikali tukio la kikatili la kutekwa na kuuawa kwa mtoto Yohana Bahati pamoja na kujeruhiwa vibaya kwa mama mzazi wa marehemu na watu wasiofahamika.
 
Akizungumza kwa masikitiko makubwa jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli amewataka Watanzania kuishi kwa amani na upendo na kuacha dhana ya kutajirika kutokana na viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
 
“Tukio hili ni la kinyama na halikubaliki popote duniani, watu wanatakiwa waelewe kuwa mtu huwezi kutajirika kutokana na viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi kama alivyofanyiwa mtoto Bahati,” alisema Waziri Magufuli.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Magufuli ametoa msaada wake wa awali kiasi cha Sh milioni moja kwa ajili ya kumsaidia Ester Jonas mama mzazi wa mtoto huyo aliyeuawa na watu hao wasiofahamika.
 
“Nimeona nitoe msaada wangu wa awali kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumsaidia mama huyu aliyejeruhiwa vibaya kwa ajili ya mahitaji yake mbalimbali na hapo baadaye nitakapopata nafasi nitakwenda nyumbani kwake kutoa pole zaidi,” alisema Waziri Magufuli.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI