TAMBWE AMSHAWISHI STRAIKA MPYA WA SIMBA


Laudit Mavugo (kushoto) Straika anayetarajiwa kusajiliwa na Simba, (kulia) mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe 

STRAIKA wa Yanga, Amissi Tambwe, amemshauri straika mwenzake, Laudit Mavugo, kuwa atakapotua Simba ajitume zaidi huku pia akisisitiza ni mchezaji ambaye anaweza kusaidia Simba kwa kiasi kikubwa.
Mbali na hilo, Tambwe amemfungukia straika huyo ambaye ilielezwa kwamba jana Jumatano angesaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba kuwa ndani ya klabu hiyo kuna ubabaishaji mkubwa ambao anaweza kukutana nao endapo tu ataonyesha kiwango cha chini tofauti na walivyotarajia.
Mavugo alifuatwa Burundi na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch ambaye ilidaiwa kuwa angemsainisha mkataba huo baada ya kukwama kuja nchini wiki iliyopita kutokana na majukumu ya kikosi chake cha timu ya Taifa.
Tambwe ambaye msimu uliopita aliichezea Simba na kuachwa katika usajili wa dirisha dogo, aliliambia Mwanaspoti kuwa kiwango cha Mavugo ni kizuri ili mradi apate ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wachezaji na viongozi wa Simba.
“Simba ni timu nzuri sana ina wanachama na mashabiki wazuri, ila tatizo lipo kwa viongozi ambao wengi wanaonekana kuwa wababaishaji na kama wataendelea na ubabaishaji wao hawatafika popote, naamini Mavugo atawasaidia sana kwani ni mchezaji mzuri na anajitambua,” alisema Tambwe.
Tambwe aliweka wazi kwamba kabla ya Mavugo kufikia makubaliano na viongozi wa Simba alimuuliza juu ya mfumo wa soka la Tanzania.
“Aliniuliza alipopigiwa simu tu, nilimwambia ukweli kwamba soka la Tanzania ni zuri ila lina changamoto kubwa kutoka kwa viongozi wa klabu anayokwenda,” alisema.
“Namfahamu Mavugo alipokuwa akicheza hapa na baadaye kwenda Rwanda, ndio maana alipopigiwa simu aliniuliza mambo mbalimbali kuhusiana na Tanzania, ni kweli angekuja huko ila kocha wetu wa timu ya Taifa alimwambia wazi kwamba angeamua kuja Tanzania kumalizana na Simba na kuacha timu ya Taifa basi huo ungekuwa ndiyo mwisho wake wa kuichezea timu hii, ndio maana hakuja.
“Kikubwa nilichomshauri ni kujituma na kufanya kazi iliyompeleka akisikiliza maneno basi anaweza kuvurugikiwa na asifanye vizuri.
“Nilimtaka ajitambue na kuongeza juhudi zaidi maana mashabiki wa Tanzania ukiharibu kidogo nao hawachelewi kukugeuzia, ila Simba ni timu nzuri tatizo ni viongozi.”
Simba inamsajili Mavugo ambaye ni raia wa Burundi akitokea Vital’O ya Burundi ingawa kabla ya kutua katika timu hiyo aliwahi kuzichezea Kiyovu na Polisi za Rwanda.
Mavugo mwenye mabao 32 msimu huu, anakuwa mchezaji wa tano wa kigeni wa Simba baada ya Emmanuel Okwi, Juuko Murshid, Raphael Kiongera na Simon Sserunkuma.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA