IJUE AFYA YAKO: HATARI YA KUTONYONYESHA

Na Dk. Richard Zuberi

Mimi niliye mdogo kwenu nimeona vema sana kwamba kila Jumatano kwa kadri Mungu atakavyotuwezesha tutakuwa pamoja katika darasa huru lenye kichwa “MEZANI KWA TABIBU”. Yale tutakayoshirikishana hapa katika meza hii sio FACT yote kabisa, kila siku kuna tafiti mpya zinafanywa na matokeo na maarifa mapya yanapatikana kwa hiyo uwe huru kuchukua cha kukufaa na kuacha kisichokufaa.

Jumatano hii ya kwanza, tutaangalia kwa sehemu tu hatari ya kutonyonyesha mtoto. Katika jamii yetu sasa kuna maendeleo makubwa sana tumeyapata ikiwa ni pamoja na mama zetu wa sasa kuwa na majukumu makubwa ya kutafuta fedha zaidi ya kulea watoto/familia na wakati mwingine kushindwa kunyonyesha watoto wao. Lakini pia kuna kundi la wamama wa kisasa ambao wameamua tu kwamba hawataki kunyonyesha kwa sababu tu za kuogopa kupoteza muonekano wao wa nje hasa matiti kupoteza shape nzuri.
Wakati mwingine tumeona tu kwamba kwa kuwa kuna maziwa ya viwandani ambayo yanapatikana na kwa kuwa tuna pesa ya kununua basi hakuna haja ya kunyonyesha. Shirika la afya duniani (WHO) linapendekeza kwamba mtoto anyonyeshwe kwa kpindi kisichopungua miezi 24 na anyonyeshwe maziwa ya mama tu bila chakula kingine kwa miezi 6
Kwa kifupi hatari za kutonyonyesha zipo kwa mtoto na kwa mama
A. Hatari kwa mtoto
1. Kuongezeka hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa mfano magonjwa ya homa ya mapafu, magonjwa ya maambukizi katika masikio, kuharisha, nk. Hii ni kutokana na kukosa kinga ambayo inapatikana ndani ya maziwa ya mama.
2. Kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama unene unaopitiliza na kisukari
3. Hatari ya kupata saratani ya damu
4. Hatari ya kupata magonjwa ya allergies mbalimbali mfano pumu na magonjwa ya ngozi
5. Hatari ya mtoto kufa kwa ghafla (sudden infant death syndrome)
6. Kiwango cha akili kuwa chini na kuwa nyuma kiutendaji wa ubongo, mfano mtoto kuchelewa kutembea, kuchelewa kuongea, kuwa mzito kuelewa darasani nk
B. Hatari kwa mama
1. Hatari ya kuwa na uwezekano wa kupata saratani ya matiti
2. Hatari ya kuwa na unene unaopitiliza
3. Hatari ya saratani ya via vya uzazi (ovarian cancer)
Baada ya kusema hayo naomba nisisitize nimetumia neno “hatari” yaani “risk” kuonesha kwamba sio lazima mtoto ambaye hajanyonya maziwa ya mama kwa muda stahiki au mama ambaye hajanyonyesha atapata hayo matatizo. Pia kwamba mtoto amepata maziwa ya mama haina maana hawezi kupata haya matatizo. Tafiti zinaonyesha bado hakuna uhusiano wa uhakika sana kati ya baadhi ya matatizo hapo juu na kutonyonya au kutonyonyesha na kwamba kuna mambo (factors) mengine yanaweza kuchangia mama au mtoto kupata madhara tajwa hapo juu.
Ahsanteni.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA