PROFESA MUHONGO AUMBUKA CCM MAKAO MAKUU



Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Waziri aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliumbuka  baada ya Chama chake kukataa kupokea lundo la makasha ya CD (santuri) zenye picha za wadhamini wake 675.

Badala yake, alielezwa kwamba, hakuna kipengele kinachoruhusu kuwa na kumbukumbu hiyo.

Profesa Muhongo, alirejesha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, saa 9:57 asubuhi na kumkabidhi Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatibu kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Baada ya kukabidhi fomu za wadhamini wake katika mikoa 15 aliyopita, Profesa Muhongo alitoa pia makasha 15 yenye CD za picha ambazo alidai amefanya hivyo ili kuonyesha hajapita njia ya mkato akidai anaamini mtu sahihi atakayeweza kuwavusha watanzania kwa sasa, ni yeye na si mgombea mwingine kati ya makada wote waliojitokeza kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.

Alipomaliza kuzungumza na kisha kukabidhi CD hizo, Khatibu alisema:”Bahati mbaya katika Daftari la kurejesha fomu za CCM za kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015 hakuna mahala panapoonyesha kwamba utapaswa kukabidhi CD ulizonipa…wanaangua (vicheko).”
 
Baada ya kuelezwa hivyo, aliondoka na kuziacha CD hizo kwa Khatibu.

Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini, baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye kutangaza nia ya kugombea urais.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA