MESSI AIZINDUA STUPANZA USINGIZINI


Mshambuliaji wa Simaba Ramadhani Singano 'Messi' 

WAKATI sakata la kiungo mshambuliaji wa Simba, Ramadhani ‘Messi’ Singano dhidi ya uongozi wa klabu yake likizidi kushika kasi kwa pande hizo mbili kutunishiana misuli juu ya ukweli wa mkataba baina yao, Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza) kimefanya jambo la maana.
Uongozi wa chama hicho umetangaza kuwaita wachezaji wote nchini katika semina ya siku moja ili kuwapiga msasa wakati dirisha la usajili likiwa limefunguliwa kwa lengo la kuwazindua kujua haki zao na kuepuka kuingizwa chaka kama inavyofanywa na baadhi wa viongozi wa klabu nchini.
Katibu Msaidizi wa Sputanza, Abeid Kasabalala aliliambia Mwanaspoti, semina hiyo ya siku moja itafanyika jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuwasaidia wachezaji kuzitambua haki zao na kupewa darasa la kusoma mikataba wanayoingia na klabu zao kabla ya kuisaini kuepuka kulizwa.
“Kwa sasa tunaendelea na mchakato wa kusaka wadhamini wa kutusaidia kuendesha semina hiyo ili kuwasaidia vijana wetu, tumebaini wengi wamekuwa wakiingia mkenge kwa kusaini mikataba kwa kuonyesha sehemu ya fedha watakazolipwa na eneo la kuweka dole gumba, lakini hawaisomi na kuielewa mikataba na wamekuwa wakiumizwa sana na klabu zao,” alisema.
Alisema kwa utafiti wao wa muda mrefu, wamebaini asilimia zaidi ya 70 ya wachezaji wanasainishwa na kupewa nakala za mikataba badala ya mikataba halisi kama inavyopaswa, ikiwa na maana wakati wa usainishwaji zinatakiwa nakala halisi tatu, ya mchezaji, klabu na ile inayokwenda TFF.
Kiongozi huyo alisema Sputanza imekuwa ikiwahamasisha wachezaji kujiunga uanachama ili kuwasaidia wanapopatwa na matatizo kama ilivyomtokea Messi, lakini wamekuwa wakihadaiwa na ujana, kitu ambacho kimekuwa kikiwaumiza na kulizwa na viongozi wajanja.
Kasabalala alidokeza kuwa, mbali na Messi, chama chao kina kesi nyingine kadhaa za wachezaji wa Ligi Kuu waliolizwa na klabu zao na wanazifanyia kazi kuhakikisha wanapata haki zao stahiki, huku wakiwahimiza wachezaji kutokosa semina hiyo itakapoitishwa wiki mbili zijazo.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA