STRAIKA MPYA SIMBA NI NOMA


                                      Straika Laudit Mavugo 

SIMBA achana nao kabisa, kwani wamefanya kitu ambacho hakuna aliyetarajia katika usajili wao wa msimu ujao.
Klabu hiyo iliamua kumfungia safari straika mkali wa Vital’O mpaka Burundi na kisha kumsainisha. Straika huyo, Laudit Mavugo amesaini mkataba wa miaka miwili.
Na kama ulikuwa hujui ni kuwa mchezaji huyo amesajiliwa kwa kitita cha Dola za Kimarekani 20 elfu na mshahara wa Dola 1,000 ambazo ni kama Sh. 2.2 Milioni. Dau alilosajiliwa na mabosi wa Msimbazi limeongeza thamani ya mchezaji huyo kinara wa mabao wa Ligi ya Burundi kwani kabla ya hapo alikuwa akiichezea Vital’O kwa dau linalokadiriwa Sh. 4 Milioni na mshahara wa Sh. 400,000 tu. Hujakosea ni Laki Nne tu!
Inaelezwa kuwa mabosi wa Simba waliamua kutoboka kiasi hicho cha fedha kutokana na kukubali ukali wa Mavugo ambaye wanaamini akiungana na Mussa Mgosi na Emmanuel Okwi pale mbele ni wazi wapinzani wao katika Ligi Kuu msimu ujao lazima waseme po!
Kusajiliwa kwa kitita hicho na mshahara atakaopokea Mavugo unamfanya kuingia kwenye orodha ya wachezaji wanaovuta mshahara mnono Msimbazi na kupandisha thamani ya maisha yake kwani inaelezwa kuwa nchini Burundi wachezaji wengi hulipwa fedha kidogo japokuwa uwezo wao kisoka ni mkubwa na imetajwa kwamba ni Vital’O ndiyo yenye kuongoza kwa kulipa wachezaji vizuri.
Mavugo amefikisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni ndani ya Simba akiwemo Emmanuel Okwi, Simon Sserunkuma, Juuko Murshid na Raphael Kiongera, huku ikielezwa kuwa Simba kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho ya kunasa beki mwingine mkali kutoka Burundi.
Beki huyo ni Nimubona Emiry ambaye amefuatwa na mmoja wa vigogo wa Simba mwishoni mwa wiki ili kuja kuungana na Hassan Kessy au Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Simba wanafanya hivyo wakisikilizia ombi la klabu kwa TFF juu ya kutaka kuongezwa idadi ya wachezaji wa kigeni.
Klabu zimekuwa zikitaka idadi ya wachezaji wa kigeni iongezwe toka watano wa sasa hadi 10 au angalau iwe saba, ombi ambalo inadaiwa kuwa lipo katika hatua nzuri kukubaliwa.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA