YANGA YAMCHOMOA NIYONZIMA, MGAMBIA ABUGI



Haruna Niyonzima
SIMBA imelazimika japo kwa shingo upande kuchomoa jina la kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima kwenye jalada la usajili wao lakini hakuna uwezekano wa Mgambia Omar Mboob kuvaa jezi Msimbazi msimu huu, Mwanaspoti limebaini.
Matajiri wa Mnyama walifikiria mkataba wa mchezaji huyo uko chini ya miezi sita ili waununue kirahisi lakini baada ya kujua ni miezi sita wakaamua kumuweka pembeni kwavile walihofia kwamba Yanga ingewakomoa, lakini mchezaji huyo alishamalizana kwa kiasi kikubwa na watu wa Simba na kuna uwezekano mkubwa akasaini Msimbazi baadae mwezi ujao tayari kwa msimu ujao.
Lakini uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope umeiambia Mwanaspoti kuwa hawatamsajili Haruna wala mchezaji yeyote mpya wa kigeni akiwepo Mgambia aliyekuja kwenye majaribio, Omar Mboob labda wawafikirie kwa msimu ujao.
Hanspope aliiambia Mwanaspoti jana kwamba: “Tayari tuna wachezaji watano wa kigeni baada ya kumsajili Dan Sserunkuma (raia wa Uganda) na kusitisha mkataba wa Mshambuliaji wetu Raphael Kiongera (Mkenya) ambaye ameondoka nchini kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.
“Labda Mboob ni kwa ajili ya msimu ujao lakini hiyo ni kama akionyesha kuwa ana uwezo wa kiuchezaji wa kiprofesheno na iwapo ataweza kuonesha hivyo basi tutakaa naye mezani na kuzungumza baada ya msimu huu kumalizika,” alisema bosi huyo mwenye ushawishi mkubwa Msimbazi.
Mboob ameingia nchini wiki hii na amepewa mechi tatu za kirafiki za majaribio ambapo moja amecheza juzi Jumatano Simba ilipocheza na Simba B, nyingine atacheza leo Ijumaa dhidi ya Express ya Uganda na mechi yake ya mwisho itakuwa dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa keshokutwa Jumapili.
Habari za ndani ya kamati ya usajili ya Simba zinasema kwamba kamati hiyo imeweka kando usajili wa wachezaji wote waliokuwa wanawawania na sasa imepanga kufunga usajili wake na kipa mmoja pamoja na beki wa kati wenye uzoefu.
Tayari Mwanaspoti linajua kwamba Simba inafanya mazungumzo na klabu ya Mtibwa Sugar ili wamchukue kipa wao, Said Mohammed (ambaye aliwahi kuchemka Yanga) kama zoezi lao la kumpata, Juma Kaseja wa Yanga litashindikana.
Pia inachonga dili kuwashawishi Azam wawape Said Morrad ili nao wawape, Haroun Chanongo. Habari ya kuwasajili Ame Ally, Salim Mbonde wote wa Mtibwa, Deus Kaseke wa Mbeya City na wachezaji wa Prisons, Nurdin Chona na Salum Kimenya wameipiga chini kwanza.
Akizungumzia kikosi hicho, kocha mkuu wa Simba, MzaPatrick Phiri alisema: “Mpaka sasa timu ipo vizuri na tatizo lililopo ni kwenye beki ya kati na mlinda mlango mmoja wote wawe na uzoefu kwa sababu kwenye ushambuliaji na sehemu nyingine ziko vizuri.”
“Nahitaji beki mwenye uzoefu pale tunaye Owino (Joseph) peke yake endapo litatokea tatizo akaumia itakuwa shida, Isihaka (Hassan) na Mgeveke (Joram) ni wazuri lakini wanahitaji msaidizi mwingine,”alisema.


“Upande wa kipa yupo, Manyika (Peter) peke yake na Ivo (Mapunda) Casillas (Hussein Sharrif) bado ni mgonjwa hatutakuwa naye, hivyo litakapotokea tatizo mmoja wao akaumia au akapata matatizo mengine kati ya hao wawili waliobaki, itakuwa shida,”alisema kocha Phiri.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI