MTUHUMIWA NAMBARI MOJA WA ESCROW HUYU HAPA



Singa singa ambaye ni mmiliki wa mtambo wa kufua umeme wa IPTL, Harbinder Singh Sethi! (wa pili kulia) akielekeza jambo.

Anaitwa Harbinder Singh Sethi! Ni mfanyabiashara bilionea mwenye asili ya Bara la Asia na mmiliki wa mtambo wa kufua umeme wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ambayo hivi karibuni imezua tafrani Bongo kufuatia kampuni yake kuhusishwa na uchotwaji wa fedha kiasi cha Sh. Bilioni 306 kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Harbinder ambaye ni singasinga anatajwa pia akidaiwa kuwa mfanyabiashara tapeli kufuatia vitendo vyake mbalimbali katika kumiliki makampuni na ukwepaji wa kodi ya serikali.
HISTORIA YAKE FUPI
Harbinder anatajwa na vyanzo kwamba ni mzaliwa wa Mkoa wa Iringa. Mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 20 ya kuzaliwa na nduguze wawili, Nota Singh na Manjit Singh walianzisha kampuni ya ujenzi wa barabara iliyojulikana kwa jina la Ruaha Concrete Co. Ltd ikitumia SLP 498, Iringa. Ruaha ni sehemu maarufu kwenye Manispaa ya Mji wa Iringa kukiwa na vitongoji vya Ipogoro, Kibwabwa na Ndiuka. Jina la Ruaha linatokana na Mto Ruaha kupita eneo hilo. 
Vyanzo vinasema, Harbinder alianza kumiliki fedha nyingi kuanzia miaka ya 80 wakati familia ya Rais wa Kenya wakati huo, Daniel Arap Moi ilipoanza kujiingiza kwenye biashara mbalimbali.
    Waziri mkuu, Mh. Mizengo Pinda.

AHAMIA KENYA
Vyanzo vikadai kuwa, miaka hiyo, singasinga huyo alihamia jijini Nairobi, Kenya ambako alianza kuwa mshirika wa kibiashara na mtoto wa kwanza wa Rais Moi aitwaye Gideon Moi.

ALIANZA UMEME NCHINI KENYA
Akiwa nchini humo, vyanzo vinamtaja singasinga huyo kuwa alipata umiliki wa mtambo wa Westmont wa kuzalisha umeme wa megawati 47 jijini Mombasa.
Washirika wenzake katika mradi huo walikuwa Mukesh Gohil, Kamlesh Pattni, Gichuru na Mkurugenzi Mtendaji wa KPLC, Mutitu.
Singh pia anatajwa kuwa na miradi  74 iliyofungwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki kutokana na kuvurunda kama siyo kufanya vibaya.

ALIPATA MSALA KENYA
Mwaka 1997, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Mashirika Kenya ilianika udhaifu wa Ruaha Concrete katika tenda ya ujenzi wa barabara ambako kulikuwa na ucheleweshaji, kuongezeka kwa gharama pamoja na utekelezaji hafifu uliojitokeza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.

Kufuatia madai hayo, ilibidi mhandisi msimamizi wa mradi huo aliyetajwa kwa jina moja la Kitololo ajiuzulu baada ya kukataa kutia saini kuwa kazi iliyozembewa imekamilika.

ARUDI BONGO
Haikujulikana mara moja ni mwaka gani alirejea Bongo, lakini ilidaiwa kuwa tayari alishawekeza nchini huku akiwa bado ana biashara zake Kenya na baadaye alirudi jumla kutokana na misala ya kule.

KWA NINI NI TAPELI?
Singh anatajwa kuwa mfanyabishara tapeli kufuatia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kumtaja kuwa amehusika na vitendo vya ukwepaji wa kodi akitumia mbinu za ujanjaujanja.
Mfano mkubwa ni hizo bilioni 306 alizochota kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow hakuzilipia kodi na ndiyo maana Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akihutubia bunge mjini Dodoma, Ijumaa iliyopita katika mjadala huo aliamuru kodi hiyo ilipwe mara moja.
Lakini pia kwa mujibu wa TRA na Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), jamaa huyo amekuwa na tabia ya kuuza hisa kwa bei ya chini kwa makampuni mengine ili aweze kulipa kodi ndogo jambo ambalo pia ni kuonesha ni mfanyabiashara tapeli.
Jaji Werema akiteta jambo na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

Kamati ya Zitto Kabwe ambaye ni mwenyekiti wa PAC, pia ilibaini kuwa, wakati yeye alijulikana kuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya IPTL ambayo baadaye aliiuza kwa Pan African Power Solutions Limited (PAP), uchunguzi wa PAC ukaja kubaini kuwa, mwenye PAP ndiyo huyohuyo mwenye IPTL, yaani singasinga huyo. Dah!

ALIHENYESHA BUNGE LA TANZANIA
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Bongo, Ijumaa iliyopita bunge liliendeshwa hadi saa 5:00 kasoro usiku, ishu ikiwa ni kujadili yaliyotokana na Kamati ya PAC baada ya kuchunguza wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka Escrow kwenda IPTL kwa kupitia PAP.
Baadhi ya mawaziri na vigogo serikalini ambao wengine walimwaga machozi kutokana na kashfa waliyoipata kupitia Kampuni ya IPTL hawatamsahau singasinga huyo kwa vile amewaingiza kwenye kumbukumbu mbaya ya Taifa la Tanzania. Katika listi ya viongozi hao yumo Mizengo Pinda, Profesa Sopspeter Muhongo, Stephen Masele, Eliakim Maswi, Jaji Feredrick Werema na wengine wengi.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI