WASHTAKIWA MAUAJI YA DK. MVUNGI WAZUA KIZAA KIZAA MAHAKAMANI



Polisi wakiimarisha ulinzi Mahakamani 

Dar es Salaam. Washtakiwa 11 wa kesi ya mauaji ya  kukusudia ya Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk.  Sengondo Mvungi wamegoma kushuka kizimbani  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishinikiza kuelezwa jalada la kesi yao lipo wapi na imefikia katika hatua gani.
Sakata hilo limetokea leo majira ya saa 4:00 asubuhi, muda mfupi baada ya Wakili wa Serikali, Peter Njike kumueleza Hakimu Mkazi, Hellen Liwa kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa kutajwa.
Baada ya wakili Njike kueleza hayo, mshtakiwa Longishu  Losingo alidai mahakamani hapo kuwa Desemba 16,2014 upande wa mashtaka uliwaambia jalada la kesi yao lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), leo (jana) wanatuletea hadithi, tunaomba watueleze uhalisia wa kesi hii, tupo gerezani tunateseka.
Kwa upande wa mshtakiwa Masunga Makenza naye alidai kuwa yeye hafahamu sheria, kesi yao ni ya muda mrefu  na akahoji jalada likienda kwa DPP linatakiwa kukaa kwa muda gani.
Makenza alidai kuwa kesi yao ni ya kubambikiwa na kwamba ingekuwa ni kesi halisi upande wa mashtaka ungekuwa umekwisha kamilisha upelelezi wao na kwamba wao wapo tayari kushtakiwa ila kama upande wa mashtaka umeshindwa kukamilisha upelelezi mahakama iwaachie huru, wakikamilisha watawakamata tena.
Wakili wa Serikali, aliieleza mahakama kuwa wameyasikia malalamiko hayo na kwamba yote yanajikita katika kuchelewa kukamilika kwa upelelezi na kwamba watahimiza na kufuatilia upelelezi ukamilike mapema.
Jibu hilo halikuwaridhisha washtakiwa hao, mshtakiwa Longishu alisema “Tumechoka kwa kweli tumechoka hatuna ugomvi na mahakama wala magereza ila tunaugomvi na waendesha mashtaka kama wameshindwa kukamilisha upelelezi watupeleke polisi.”
Yote kwa yote washtakiwa hao, wakaiambia mahakama kuwa kutokana na hoja hizo za upande wa mashtaka leo (jana) hawapo tayari kushuka kizimbani, watakaa chini hadi waelezwe jalada leo lipo wapi na kesi imefikia katika hatua gani.
Baada ya washtakiwa hao wote kugoma kushuka kizimbani na kukaa chini wakisubiri kuelezwa hatma ya kesi yao, Hakimu Liwa aliwasihi  wakubali kuondoka kizimbani hapo kwa sababu yeye siyo hakimu husika ameitaja tu kesi yao, wamsubiri hakimu husika, Waliarwande Lema wamueleze malalamiko yao.
Maelezo hayo ya hakimu Liwa walikubaliana nayo na kwa pamoja wakainuka na kuelekea mahabusu ya mahakama kwa ajili ya kupelekwa mahabusu na kesi iliahirisha hadi Januari 13,2015.
Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Chibago Magozi (32),  John Mayunga (56),Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Zacharia  Msese (33), Msungwa Matonya (30), Ahmad Kitabu (30).
Kwa pamoja  wanadaiwa kuwa   Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha sheria na kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI