SIMBA YAMTELEKEZA KWIZERA DAR



Kiungo wa zamani wa Simba, Mrundi, Pierre Kwizera.

KIUNGO wa zamani wa Simba, Mrundi, Pierre Kwizera hivi sasa ana wakati mgumu hapa jijini Dar, kutokana na uongozi wa klabu hiyo kumtelekeza kwa kutomlipa madai yake, baada ya kumvunjia mkataba wake pamoja na mwenzake, Amissi Tambwe.
Simba iliwavunjia mikataba nyota hao kutokana na kutoridhishwa na uwezo wao uwanjani na nafasi zao kuchukuliwa na Waganda, Simon Sserunkuma na Juuko Murushid.Habari zilizopatikana ni kwamba Simba wamevunja makubaliano ya malipo yao, ambapo ilitakiwa walipwe chao tangu Desemba 17, mwaka huu lakini uongozi wa klabu hiyo umeshindwa kufanya hivyo huku wakikataa hata kupokea simu zao.
Mtoa habari alikwenda mbali na kusema kuwa kwa sasa Kwizera anatia huruma kutokana na kuwa na wakati mgumu ambapo Simba wamekuwa wakimpiga danadana kuhusu kupewa malipo yake ambayo ni dola 7000 (zaidi ya shilingi milioni 11).
“Kwizera hivi sasa anaishi maisha magumu, hana pesa kabisa hata kula kwake siku hizi kumekuwa kwa kuombaomba kwa sababu Simba hawataki kumpatia fedha zake, hata Tambwe pia hajalipwa sema yeye kidogo ana unafuu baada ya kujiunga na Yanga.“Nasikia wanasema kuwa watawalipa kuanzia Jumatatu wiki ijayo, ila sijui kama watatoa,” kilifunguka chanzo hicho.
Championi kwanza ilimtafuta rais wa klabu hiyo, Evans Aveva lakini simu yake haikupokelewa licha ya kutafutwa mara kadhaa kabla ya kumpata katibu mkuu, Stephen Ally ambaye alisema: “Hao ni waongo. Achana na hayo ya kina Tambwe, wee njoo uwanjani (jana, dhidi ya Kagera Sugar) uangalie burudani.”
Nyota hao wanaidai Simba jumla ya dola 14,000, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 22.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI