MTOTO WA AJABU AZALIWA DODOMA,SURA NUSU MTU NUSU CHURA


Mkazi wa   kijiji cha  Chibwechangula Behelo  wilaya ya Mpwapwa mkoani hapa, Ruth  Stanely  Matonya (26),  amejifungua mtoto wa ajabu wa jinsia ya kike mwenye kichwa nusu.

Mtoto huyo ambaye alikuwa na  sura inayofanana na ya chura huku viungo vingine vya mwili vikiwa vya binadamu, alifariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Tukio hilo limetokea jana katika kituo cha afya cha mtakatifu Luke  kinachomilikiwa na Kanisa la Anglikana  Dayosisi ya Mpwapwa.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,  Dk. Edwin Kihura, mama huyo baada ya kufika kituoni hapo alikuwa na uchungu  mkali ambao uliendelea bila kukoma  huku akisindwa kujifungua hali iliyosababisha afanyiwe upasuaji.

“Pamoja na uchungu huo mkali lakini hakuweza kijifungua  kwa njia ya kawaida ingawa njia ilionyesha ipo wazi mtoto aweze kutoka  tuliamua kumfanyia upasuaji ili kuokoa maisha ya mama huyu,” alisema Dk. Kihura.

 Dk.Kihura alisema maendeleo ya ujauzito wake alipokuwa akifika kliniki yalikuwa hayaonyeshi mkao wa mtoto huyo na mapigo ya moyo yalikuwa hayapatikani .

“Miezi ya mwisho mama huyu alipokuwa akihudhuria kliniki tulikuwa hatupati mkao wa mtoto  na mapigo  ya moyo yalikuwa hayapatikani lakini mtoto alikuwa anacheza tumboni kitu ambacho kilikuwa kikiwashangaza sana  waganga na wauguzi wa kituo hiki,”alisema Mganga huyo.

Alisema  baada ya kufanyiwa upasuaji walitoa mtoto huyo, akiwa na sura isiyoeleweka inayofanana na chura na  kichwa nusu.

Akizungumzia tatatizo hilo linasababishwa na nini, Mganga huyo,  alisema kuna sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na mama kukosa baadhi ya madini mwilini na hivyo uumbaji wa mtoto kutokamilika.

“Unasababishwa na sababu za kibailogia   ambazo ni kushidwa kugawanyika kwa kromozome na tatizo kama hili limewahi kutokea  mara chache sana

katika hospitali nyingi lakini vitendo hivi vimekuwa vikiongezeka  kwa wingi siku hizi za karibuni na kitaalamu linajulikana kama ANECEPHALY,”alisema  Mganga huyo.

Aliitaja sababu nyingine kuwa ni baadhi ya kina mama kutumia dawa za kienyeji ambazo ni kali wakati mimba zikiwa changa zinaweka sumu kwa mtoto tumboni.

Alisema hali ya mama huyo inaendelea vizuri katika  kituo cha mtakatifu  Luke ambako anaendelea kupatiwa matibabu.
SOURCE: NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA

MAGONJWA 27 YANAYOTIBIWA NA ASALI YENYE MDALASINI