UTABIRI WA HALI YA HEWA: MVUA KUBWA, TAHADHALI KWA MIKOA HII TISA
Maeneo kadhaa ya kaskazini magharibi mwa Tanzania yameanza kushuhudia mvua kubwa kufuatia angalizo lililotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Angalizo hilo linahusu uwezekano wa mvua kubwa kunyesha katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kigoma, Tabora na Katavi. Mvua hizo zinatarajiwa kuendelea kunyesha hadi Jumanne, machi 8.
Kwa mujibu wa TMA, mvua hizi zinaweza kuambatana na upepo mkali na ngurumo za radi, hali inayoweza kusababisha madhara kama mafuriko ya ghafla, ucheleweshaji wa usafiri na uharibifu wa miundombinu, hasa katika maeneo yenye miinuko au yenye mifereji mibovu ya maji.
Wakazi wa maeneo hayo wameaswa kuchukua tahadhari zote muhimu, ikiwa ni pamoja na kuepuka maeneo hatarishi wakati wa mvua, kuimarisha makazi yao dhidi ya upepo mkali na kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa.
Mvua hizi ni sehemu ya mfululizo wa mvua za masika zinazotarajiwa kuendelea kwa wiki chache zijazo katika baadhi ya maeneo ya nchi. Hata hivyo, TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na itatoa taarifa zaidi kadri hali inavyoendelea kubadilika.
Serikali za mitaa na vyombo vya uokoaji vimeombwa kuwa tayari kushughulikia matukio yoyote ya dharura yatakayojitokeza. Wananchi pia wametakiwa kushirikiana kwa kutoa taarifa za mapema kuhusu maeneo yaliyoathirika.
Comments
Post a Comment