BAADA YA MUALIKO WA SIMBA: MWAMPOSA ATOA KAULI HII


Mtume Boniface Mwamposa amekiri kupokea mwaliko wa klabu ya Simba kama Mgeni Maalum kuelekea mchezo wa Simba dhidi ya Al Masry, ambapo ameweka wazi kuwa hiyo ni ishara ya kuzidiwa kwa waganga. Mwamposa aliongeza kuwa hata wachezaji wanamkuta na ameombea wengi akiwemo Fiston Mayele.

Akizungumza kupitia ibada ya Aprili 6, 2025 kwenye Kanisa lake la Arise And Shine Jijini Dar es salaam, Mtume Mwamposa alisema kuwa yeye ni kiongozi wa vilabu vyote na watu wote. Ambapo habagui na wala asidhaniwe kuwa ni shabiki wa Simba baada ya mwaliko.

Mwamposa aliweka wazi kuwa kama hatapata nafasi ya kuhudhuria mwaliko huo itabidi atume mwakilishi, kwani ana mambo mengi mbele yake kwa sasa. Lakini huduma ya maombi ikihitajika ataitoa kwa klabu hiyo ilikusudi kwa nguvu za Mungu ipate ushindi.

Mtume huyo alionyesha hali ya kufurahishwa na mwaliko huo, kwa maana anaamini kuwa ni ishara ya kudoda kwa waganga wa kienyeji. Huku Mungu akionekana kung'aa zaidi eneo la michezo hasa mpira wa miguu nchini. Jambo ambalo halikuwa vile miaka ya nyuma kidogo.

Huku akisema kuwa kwa sasa wachezaji wengi anawaombea, ambapo mfano mzuri ni Fiston Kalala Mayele ambaye alijitokeza hadharani licha ya kuombewa kwa siri. Ikumbukwe kuwa, Mayele kwa sasa ni tishio barani Afrika, pia kwenye klabu yake sasa.

Jambo ambalo limeibua gumzo kubwa kwa mashabiki wa mpira nchini, ambapo baadhi wanaamini kuwa kupitia Mwamposa klabu ya Simba itafanya vyema dhidi ya Al Masry. Huku baadhi wakiamini kwamba ni juhudi pekee ndiyo zitakazo ifanya Simba itambe siku hiyo.

Je, kwa upande wako una maoni gani kufuatia mwaliko wa Mwamposa kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Al Masry? Karibu kwa maoni.

Chanzo: Simba SC Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA