MGOMBEA UBUNGE ACT-MAENDELEO AAHIDI KUWASAIDIA WANAWAKE



MTIA nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Kahama kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Clara Masanja amesema endapo atapewa ridhaa na chama hicho na kushinda nafasi hiyo, atahakikisha anawajengea wanawake ujasiri ili waweze kujipigania wenyewe katika kupata nafasi za uongozi wa juu.
 
Mgombea huyo, aliyasema hayo mjini hapa jana wakati alipotangaza nia yake ya kuchukua fomu ya kuombea kiti hicho katika ofisi za chama hicho, na kuwasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hata kama si za kisiasa.
 
Masanja anayesomea shahada ya kwanza ya ufamasia katika Chuo Kikuu cha Kampala nchini Uganda, alisema akiwa kama mwanamke ataonyesha mfano kwa wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, hasa katika wilaya hiyo, ambayo haijawahi kupata mbunge mwanamke.
 
“Nitakapochaguliwa kuongoza jimbo hili la Kahama, nitahakikisha pia naondoa kero mbalimbali katika Idara ya Afya,” alisema mgombea huyo ambaye pia alikuwa mtumishi katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga katika ngazi ya ufamasia daraja la pili.
 
Alisema kabla ya kuamua kugombea kiti hicho, aliona jimbo hilo lina changamoto nyingi zilizopo katika jamii, kama vile wananchi kutopata haki zao za msingi katika mambo mbalimbali ya kijamii.
 
Aidha, alisema makundi mengi ya watu hususani wazee wamekuwa hawapati msaada wa kutosha hospitalini licha ya Serikali kutangaza matibabu kwa wazee ni bure hali inayoweka kundi hilo katika wakati mgumu wa kupata matibabu pindi wanapoumwa.
 
“Wazee wakienda Hospitali pamoja na kuambiwa matibabu ni bure, hujikuta wakiambiwa kuwa hakuna dawa na kulazimika kununua dawa hizo kwenye maduka ya nje yanayomilikiwa na madaktari wa hospitali husika,” alisisitiza.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA