MCHAKATO WA URAIS: TANO BORA ITATOKA KWENYE KUNDI HILI HAPA




WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya RaisKamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo inakutana kuchuja majina ya makada wake 38 waliorejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho na majina 33 ni lazima yapigwe panga ili kupeleka majina matano kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupigiwa kura.

Kwa mujibu wa habari kutoka mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe na mijadala sehemu mbalimbali, majina hayo matano yanaaminika kwamba yatatoka miongoni mwa watiania 10 ambao wametajwa zaidi katika mijadala hiyo.

Sababu kuu mbili ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye mijadala hiyo na hata na baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa Tanzania ni mbili. Mosi, uzoefu wao ndani ya ungozi wa serikali na pili, nafasi yao ndani ya chama, ama kama wajumbe wa NEC au Kamati Kuu.

Majina ambayo yanatazamiwa kwamba yanaweza kupenya Kamati Kuu ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli;.

Kwa ujumla kundi la makada hao (hapo juu) kila mmoja ana nafasi ya kupenya kwenye mchujo wa Kamati Kuu, lakini pia anakabiliwa na changamoto kadhaa.
 
Bilal
Dk. Bilal ni Makamu wa Rais, katika hali ya kawaida ni vigumu msaidizi namba moja wa rais aliyeko madarakani kukosa nafasi ya kupenya ngazi hiyo hata kama ni kwa sababu tu za kiprotokali .

Mbali na wadhifa wake, Bilal anayetoka Zanzibar amepata kuwa Waziri Kiongozi na ana uzoefu wa kuendesha serikali, kwa maana hiyo anawakilisha kundi la upande mmoja wa Muungano na hivyo siyo rahisi jina lake kutokuzingatiwa.
  
Hata hivyo, Bilal ana changamoto ya umri kwani kwa umri wa miaka 70 alio nao sasa inakuwa ni kazi kubwa kukimbizana na changamoto za sasa katika nafasi hiyo.

Lowassa
Lowassa ni mbunge wa Monduli, lakini pia alipata kuwa Waziri Mkuu hadi alipojiuzulu Februari 2008 kutokana na kadhia ya Richmond juu ya mkataba wa kufua umeme. 
  
Hata hivyo, kadri muda ulivyosonga hadi sasa kadhia hiyo ilikuja kujidhihirisha kusukumwa zaidi na misuguano ya ndani ya CCM hasa juu ya chuki za nafasi ya uwaziri mkuu.

Kama walivyo watia nia wengi, ni mjumbe wa NEC, amekuwa waziri katika serikali ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na ya Rais Benjamin Mkapa, anaijua serikali vizuri.

Lowassa amekuwa gumzo kubwa miongoni mwa watia nia wote kiasi cha kuandamwa hata na wapinzani wake ndani ya chama kwa kuwa tu kila wakati kura za maoni zimeonyesha kuwa ni chaguo la kwanza la wananchi katika kundi la wawania urais wote, ndani ya CCM na hata ndani ya upinzani.

Mwanasiasa huyo ambaye wengi waliamini kwamba kadhia ya Richmond ilikuwa imemmaliza, aliigeuza hali hiyo kiasi cha kuonekana kuwa mtu anayestahili kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  
Mvuto wake kwa wananchi wengi, umefanya wapinzani wake wajipange kumwandamana kwa tuhuma mbalimbali, ambazo amezipuuza.

Wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini ndani ya CCM, Lowassa alionyesha kwa vitendo halisi jinsi anavyoungwa mkono na wanaCCM wenzake, kwani mikutano yake iligeuka kuwa ‘mafuriko’ kila mkoa alikokwenda. Alidhaminiwa na wanachama zaidi ya laki nane.

Lowassa anaungwa mkono na wananchi wengi kwa sababu ni miongoni mwa viongozi wa serikali wachache ambao wanatenda kwa vitendo halisi kuliko kupiga kelele kwenye majukwaa ya kisiasa.

Anakumbukwa kwa ufuatiliaji wa karibu kwenye kila wizara aliyokuwa, anakumbukwa kwa kusaidia Tanzania kunufaika na maji ya ziwa Victoria na wakati akiwa Waziri Mkuu alianza kubadili mfumo wa utendaji serikalini kutoka ‘business as usual’ na kuibua ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi miongoni mwa watumishi wa umma.

Wassira
Wasira ni miongoni mwa makada wa siku nyingi wa CCM, amehudumu kama waziri katika serikali za awamu tatu, ya Mwalimu Nyerere; ya Mzee Mwinyi na ya awamu ya nne, inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

Ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe, akiwa amejizolea umaarufu ndani ya CCM na hata kwenye upinzani kwani mwaka 1995 alihamia NCCR-Mageuzi na kugombea ubunge jimbo la Bunda na kumshinda, Jaji Joseph Warioba.
  
Hata hivyo, baadaye mahakama kuu ilitengua ubunge wake na kumtia hatiani kwa kuhusika na vitendo vya rushwa katika uchaguzi.

Ingawa kiutendaji Wasira anaonekana kama mmoja wa watu wanaojituma, kitendo chake cha kuhama CCM na kurejea tena kinaweza kuwa moja ya sababu za kutumika dhidi yake.

Membe
Amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2007 alipoondoka Dk. Migiro kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).
  
Membe aliingia bungeni mara ya kwanza mwaka 2000 wakati wa utawala wa Mkapa, lakini ni chini ya Kikwete alipata nafasi ya kuwa Naibu Waziri, akianzia Mambo ya Ndani na baadaye Nishati na Madini kabla ya kuibukia Mambo ya Nje kama waziri kamili.

Ni mjumbe wa NEC kama walivyo makada wenzake. Kwa miaka mingi ya utumishi wake Membe ambaye pia ni ofisa wa usalama wa taifa, alifanya kazi nje ya nchi.

Duru za kisiasa nchini zinasema kuwa ingawa hana mizizi mirefu ndani ya chama, kukaa kwake wizara ya Mambo ya Nje kwa muda huo kumempa uzoefu wa uendeshaji wa serikali. 
  
Hata hivyo kumekuwa na maoni kuwa Membe anabebwa na wakuu serikalini.

Migiro
Huyu ni mwanamke pekee anayepewa nafasi ya kufika mbali miongoni mwa watia nia wote kwa sababu ya nafasi yake, kwanza ndani ya nchi na nje alipokuwa UN. Anaelezwa kuwa na uzoefu wa ndani na wa kimataifa.

Katika kipindi hiki ambacho Rais Kikwete amekuwa anatoa fursa nyingi zaidi kwa wanawake katika vyombo vya maamuzi, Dk. Migiro anaweza kupenya kwenye kundi la tano bora hivyo kusaka kura za NEC kama anataka kufika kwenye tatu bora kwenye mkutano mkuu.

Pinda
Huyu ni waziri mkuu tanu Februari 2008 alipojiuzulu Lowassa. Pinda amekuwa mbunge tangu awamu ya pili ya Rais Mkapa na kuwa waziri wa Tamisemi.

Muda wake mwingi wa utumishi alikuwa ndani ya Ikulu kama ofisa wa serikali. Ni mwanasiasa ambaye kimsingi hajawa na kishindo sana licha ya nafasi yake kubwa ya uwaziri mkuu.

Pinda amekuwa miongoni mwa mawaziri wakuu wapole ambao hawajaacha kishindo kama alivyokuwa Waziri Mkuu pekee wa Rais Mkapa, Sumaye ambaye alikaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 10, lakini hakuacha kishindo chochote pia.

Hata hivyo, kwa sababu za itifaki kama ilivyokwa Dk. Bilal, itakuwa ni vigumu kumpiga panga jina lake katika ngazi ya Kamati Kuu, ingawa wote umri nao umesogea, Bilal miaka 70 na Pinda miaka 67.

Mwandosya
Mwandosya ni mwanasiasa aliyeweka rekodi mwaka 2005 kwa kuingia tatu bora katika kinyang’anyiro cha urais, akiachwa nyuma na Kikwete na Dk. Salim Ahmed Salim.

Amekuwa moja ya nguzo ya siasa ya CCM kwa miaka mingi na ndiye alianzisha mkakati wa harambee ya kuchangia chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Amehudumu katika awamu mbili kama waziri, awamu ya tatu na ya nne. Kwa kitambo alikuwa ndiye nguzo ya wanaCCM mkoani Mbeya, lakini kuibuka kwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, kama mmoja wa watia nia, kumeibua maswali mengi kama Profesa Mwandosya bado anashikilia nafasi hiyo Mbeya na kanda yote ya nyanda za juu kusini. 
  
Hata hivyo, umri wa miaka 66 wa Mwandosya siyo haba katika dunia ya leo inayohitaji mchakamchaka.

Sumaye
Sumaye aliweka rekodi ya waziri mkuu aliyekalia kiti hicho mfululizo kwa muda mrefu zaidi ya mawaziri wakuu tisa kuwahi kuteuliwa tangu uhuru.

Hakuna ubishi kwamba Sumaye ana uzoefu wa kuendesha serikali, amekuwa naibu waziri, waziri na waziri mkuu kwa miaka 10. Alishikilia ubunge wa jimbo la Hanang hadi alipoamua kustaafu mwaka 2005 baada ya kuliwakilisha kwa miaka 20.

Ingawa Sumaye hana kikwazo chochote cha kisiasa kupenya hatua ya Kamati Kuu, nguvu zake za kisiasa jimboni kwake zimepungua ndiyo maana mwaka 2012 alibwagwa katika nafasi ya UNEC na Mary Nagu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahisiano na Uratibu).

Magufuli
Dk. Magufuli amekuwa ni miongoni mwa mawaziri wachache wachapakazi tangu awamu ya Rais Mkapa na hata sasa.
  
 Amekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na kisha Waziri wa Ujenzi wakati wa Mkapa na chini ya Kikwete amekuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo, kisha wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kila alikopelekwa amejitahidi kuchapa kazi.
 
Ni kati ya mawaziri wanaozijua wizara na majukumu yao sawasawa, ni mfuatiliaji. Kwa utendaji huo, Magufuli amejijengea sifa ya kuwajibika kama kiongozi.

Hata hivyo, kuna jambo kubwa ambalo limekuwa likiibuka kila wakati juu ya kuhusika kwake na uuzaji wa nyumba za serikali.
  
Ingawa inadaiwa kuwa ulikuwa uamuzi wa baraza la mawaziri, bado wananchi wengi wamekuwa wakihoji uamuzi wa kuuza nyumba hizo.

Mbali ya kuwa mbunge wa Chato tangu mwaka 1995, Magufuli hajawahi kugombea nafasi nyingine ya kuchaguliwa ndani ya CCM. 
  
Siyo mjumbe wa NEC na hakuna kumbukumbu zozote kwamba alipata kuomba nafasi hiyo.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA