MAGUFULI ATAMBULISHWA ZANZIBAR, AAHIDI KUFUATA NYAYO ZA KARUME NA NYERERE


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema endapo akifanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania, ataongoza nchi kwa kufuata nyayo za waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
 
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo mjini Unguja, Zanzibar jana, baada kupokewa na mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Ndege wa Karume, huku akiwa na ulinzi mkali tofauti na siku zote.
 
Alisema viongozi hao waliweka misingi iliyojali kila mtu jambo ambalo limesaidia kuweka umoja, amani, utulivu na mshikamano.
 
“Nawahakikishia kuwa nitafuata nyayo za waasisi wetu endapo mtanipa ridhaa ya kuongoza Oktoba, mwaka huu.
 
“Nina deni kubwa kwenu na kwa nchi yangu, eleweni hamtajutia uamuzi wa kunichagua, nitafanya kazi kwa bidii, utii na maarifa kulijenga Taifa hili bila kumbagua mtu yeyote,” alisema Dk. Magufuli         
   
Alisema Taifa lolote duniani linalopuuzia kujenga umoja, upendo na mshikanao wa kitaifa, hupoteza haiba na dhamira ya  kujenga uchumi imara.
 
Dk. Magufuli ambaye aliambatana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan, alisema atatimiza kile ambacho Watanzania wanakitegemea kutoka kwake.
 
“Nataka niseme jambo muhimu kwa Watanzania wenzangu, sikuja hapa kwa ajili ya kampeni, tambueni bila umoja, amani na utulivu hakutakuwa na mageuzi yoyote au  mikakati ya kupambana na kutokomeza  maadui ujinga, umasikini na maradhi,” alisemas Dk. Magufuli.
 
Alisema ataongozwa na ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20 ili kuhakikisha sekta ya utalii Zanzibar inakua.
 
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema anamfahamu Dk. Magufuli kuanzia mwaka 1996, akimtambua kuwa ni kiongozi mchapakazi mahiri, hodari na mzalendo.
 
Alisema kuteuliwa kwake ni kielelezo kinachothibitisha kukubalika kwa mgombea huyo ndani ya chama chake.
 
Kwa upande wake, Samia aliwasifu wanawake wenzake wawili walioingia tano bora na baadaye tatu bora; Balozi Amina Salum Ali na Dk. Asha-Rose Migiro kwa kusema ushupavu wao na umadhubuti wamewatia ari na moyo wanawake wengine nchini.
 
Mapokezi hayo yalihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha, manaibu katibu wakuu wa CCM Zanzibar na Bara, Vuai Ali Vuai na Radjab Luhavi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Unguja, Borafya Silima Juma na baadhi ya mawaziri.
 

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA