CHADEMA YAITISHA KIKAO CHA DHARURA KUJADILI ADHABU YA WABUNGE WA UKAWA WALIYOPEWA BUNGENI



Homa ya Uchaguzi Mkuu imeifanya Chadema kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ili kujadili mambo ya kitaifa, ikiwamo adhabu waliyopewa wabunge wa Ukawa kabla ya kutoa tamko. 
 
Kikao hicho kilichofanyika jana, pia kilihusisha wabunge walioadhibiwa kwa kufanya fujo bungeni wakipinga kuwasilishwa kwa miswada mitatu ya mafuta na gesi kwa hati ya dharura na hivyo kupewa adhabu tofauti ya kutohudhuria vikao kuanzia viwili hadi vyote vilivyosalia.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari, manaibu katibu mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) walisema kutokana na kuongezeka kwa homa ya uchaguzi, chama hicho kimelazimika kuitisha kikao hicho na kwenda tofauti na ratiba yake ya mwaka ili kuweka sawa baadhi ya mambo.
 
“Pamoja na ratiba iliyopo, kila litakapokuwa linajitokeza jambo muhimu tutakuwa tunaitana ili kulijadili kwa kina. Hali ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura Zanzibar ina ishara zote kuwa hatutakuwa na mwisho mzuri,” alisema Mwalimu na kufafanua kuwa kikao hicho kitakuja na jibu... “Kama hali hiyo haitarekebishwa, upo uwezekano wa athari zake kufika Bara pia.”
 
Mwishoni mwa wiki, polisi walifyatua risasi kwenye kituo cha kuandikisha wapigakura baada ya wananchi kwenda eneo hilo kujaribu kuzuia kile walichokiita “wapigakura mamluki” na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa hospitalini.
 
Mwalimu alisema majibu rahisi yanayotolewa na Serikali kuhusu vurugu hizo kuwa zinafanywa na vikundi vya wahuni, yanatia shaka hasa kwa kuzingatia kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo na vinashuhudia mambo hayo yakitokea.
 
Alieleza kuwa matukio yasiyo ya kawaida hayatokei Zanzibar pekee, bali hata maeneo mengine, akitoa mfano kwenye uandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR ambako alisema kuna hali inayokanganya hivyo kufanya kuwapo umuhimu kwa chama kutoa tamko juu ya kinachoendelea.
 
“Wale walioandikishwa mwanzo kwenye wilaya za Mlele mkoani Katavi na Kilombero, Morogoro wameambiwa warudishe kadi walizopewa na waandikishwe upya. Hii siyo hali ya kawaida na hasa inafanywa katika majimbo ambayo ni ngome ya Chadema,” alisema na kuongeza:
 
“Pamoja na hayo yote, tutatangaza ushindi mapema sana wilayani Kilombero katika uchaguzi mkuu ujao.”
 
Kuhusu kikao hicho, Mnyika alisema kilijadili maandalizi ya jumla ya Uchaguzi Mkuu, kupokea taarifa za wagombea udiwani, ubunge na urais, taarifa ya majadiliano ya Ukawa pamoja na ile ya wabunge waliopewa adhabu.
 
Akitoa msimamo wa awali wa chama chake, Mnyika alisema wabunge hao walikuwa na sababu zote za msingi za kupinga miswada hiyo na kwamba taarifa zilizoripotiwa kuwa wanatumiwa hazina mashiko yoyote.
 
“Chama kinaungana na wabunge wa Ukawa kumtaka Rais asisaini miswada hiyo. Tunazo taarifa kuwa uharakishaji huu unafanywa ili kutimiza masharti tuliyopewa na mataifa ya nje ikiwa ni pamoja na vigezo vya kupata fedha za Mfuko wa Milenia,” alisema Mnyika.

Wakati Chadema ikifanya hivyo, inatarajiwa kuwa vyama vingine vinavyounda Ukawa vitafanya vikao vyake na kufikia uamuzi ambao utawasilishwa katika kikao cha wakuu wa vyama hivyo na kujadiliwa.
 
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shawej Mketo alisema jana kuwa pamoja na vikao vya umoja huo, kila chama kina ratiba yake ya vikao vya ndani.
 
“Tutakuwa na kikao cha Baraza Kuu na Kamati ya Utendaji mwishoni mwa mwezi huu. Nadhani ni mara tu baada ya Sikukuu za Idd. Mambo yote yatajadiliwa huko,” alisema Mketo.
 
Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema chama chake kilishafanya mkutano mkuu Juni 27 na uwezekano wa kuwa na kikao kingine utakuwapo endapo kutakuwa na mgombea urais kutoka ndani ya chama hicho.
 
Kuhusu wabunge waliopewa adhabu, Nyambabe alisema kwa kuwa ndani ya Bunge yumo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye pia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wa chama chake, James Mbatia jambo hilo litajadiliwa vizuri katika kikao cha pamoja.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA