MAGUFULI ATAMBULISHWA ZANZIBAR, AAHIDI KUFUATA NYAYO ZA KARUME NA NYERERE
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema endapo akifanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania, ataongoza nchi kwa kufuata nyayo za waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo mjini Unguja, Zanzibar jana, baada kupokewa na mamia ya wananchi kwenye Uwanja wa Ndege wa Karume, huku akiwa na ulinzi mkali tofauti na siku zote. Alisema viongozi hao waliweka misingi iliyojali kila mtu jambo ambalo limesaidia kuweka umoja, amani, utulivu na mshikamano. “Nawahakikishia kuwa nitafuata nyayo za waasisi wetu endapo mtanipa ridhaa ya kuongoza Oktoba, mwaka huu. “Nina deni kubwa kwenu na kwa nchi yangu, eleweni hamtajutia uamuzi wa kunichagua, nitafanya kazi kwa bidii, utii na maarifa kulijenga Taifa hili bila kumbagua mtu yeyote,” alisema Dk. Magufuli ...