LOWASA : TUHUMA ZA KUWALIPA WATU WANISHAWISHI KUGOMBEA URAIS NI UPUUZI NA UONGO


Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amesema watu wanaosema anawalipa watu wanaomshawishi awanie nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, ni upuuzi na uongo na kwamba hawezi kuwajibu kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili.

Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana mjini Dodoma, kufuatia baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, akisema baadhi ya watu wanatumia vibaya umaskini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.

Akizungumza mbele ya wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya kuwagharimia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi na kwamba wengi wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.

“Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja) kusema leo (jana) kuna mtu kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo kidogo, ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu,” alisema.

Alisema makundi yanayomshawishi awanie nafasi hiyo wanafanya hivyo kwa utashi wao, mapenzi yao kwa taifa na Mungu wao na kwamba ‘lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo.’

Awali, Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa wanalipwa, ni walioishiwa hoja, wamefilisika na sasa wanatapatapa na kwamba kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.

“Nimekaa muda mrefu kwenye siasa, wengine bado wanahitaji wapate muda wa kujifunza na katika siasa hatuwajui ni wapi walipotokea, wakipata muda mzuri wajifunze, wawe na adabu, watulie kuliko kuzusha maneno ambayo huna uhakika nayo, ambayo ni dhambi kubwa sana,”alisema Mgeja. 
 
Alisema wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya siyo makosa.

“Tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi. Kama viongozi tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka mbele, niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna mwingine zaidi ila Mheshimiwa Lowasa,” alisema Mgeja.

Aidha, Lowassa alizungumzia ujio wa wachungaji hao nyumbani kwake jana, akieleza kuwa umeandika historia katika maisha yake kwani hakutegemea kupokea kundi kubwa kama hilo la watumishi wa Mungu.

Alisema watu ambao wamemfuata kumshawishi amewaambia kuwa nafasi ya urais ni kubwa na inahitaji maombi.

“Ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu,” alisema.

Mapema, Mratibu wa ujio wa Wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.

“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.

Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.

Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi, Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni, Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.

Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe, Mwibara, Kisarawe, Nachingwea na Kilolo.

Wanafunzi,Wafanyabiashara  wanena.
Wakati huo huo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara mjini Dodoma waliokwenda kwa Lowassa juzi kumshawishi agombee, wamesema kwa Lowassa hakukuwa na ubwabwa wala soda na kwamba kauli ya Makamba inaonyesha kuwa Lowassa ni kiongozi anayefaa ndio maana watu wanampinga.

Rais wa Kitivo cha Imformative katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Goodluck Philip, alisema wanafunzi walikwenda kwa Lowassa kwa utashi binafsi na bila shinikizo na kwamba kauli ya kuhongwa imewadhalilisha.

Alisema kauli hizo zinalenga kuwatisha watu wakati msingi wa kufanya hivyo ni wa kidemokrasia.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Dodoma, Norbati Pangaselo, alisema wapinzani wa Lowassa wanatakiwa kujenga hoja badala ya kuzusha uongo kwa nia ya kumchafua.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA