WACHEZAJI SIMBA WAMPA NENO MZUNGU
UTAMADUNI wa Simba miaka yote ni kucheza soka la kushambulia. Wachezaji wa timu hiyo wameangalia staili ya uchezaji ya timu hiyo kwa sasa wakaamua kumwelezea kocha wao Mserbia Goran Kopunovic ukweli ambao huenda ukasaidia kulinda kibarua chake.
Beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye aliyekuwa wa kwanza. Amemwambia kocha huyo kwamba anafurahishwa na soka la kushambulia kwani linamwongezea uhuru wa kucheza.
Tangu kuwasili kwa Goran, Simba imeonekana kucheza soka la kushambulia zaidi huku ikiwatumia mabeki wake wa pembeni, Tshabalala na Hassan Kessy zaidi kama nguzo hiyo ya mashambulizi kwa kusaidiana na mawinga.
Tshabalala alisema aina hiyo ya soka inamwongezea uhuru wa kucheza kwani muda mwingi anapenda kupanda kwenda kusaidia mashambulizi ya timu yao. “Napenda kupanda kwenda kusaidia timu katika mashambulizi, kwa staili ya kocha huyu( Goran Kopunovic) napata uhuru wa kucheza kwa kufunguka zaidi, kocha anapenda tushambulie,” alisema Tshabalala
Mbali ya hilo, beki huyo alisema fursa aliyopata ya kuaminiwa na kupewa nafasi katika kikosi cha kwanza inamwongezea nguvu za kupambana kwani anafahamu fika kuwa akiteleza nafasi yake itapotea kikosini hapo.
“Najua nje ya uwanja kuna wachezaji wazuri, wanatamani kucheza kama mimi hivyo muda wote ninaokuwa uwanjani nacheza nikiwa na hilo akilini, najitahidi pia kukumbuka majukumu niliyopewa na kocha,” alisema Tshabalala
Beki huyo anakuwa miongoni mwa nyota wachache waliosajiliwa na Simba msimu huu na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo akiwapiku mabeki wenzake Issah Rashid ‘Baba Ubaya’ na Abdi
Banda. Tshabalala amecheza mechi zote za Liigi Kuu msimu huu hadi sasa pamoja na zile za Kombe la Mapinduzi.
Mkude: Kombinesheni imeiva
Kiungo wa Simba, Jonas Mkude amesema kwa sasa kombinesheni yake na kiungo Said Ndemla imeiva na wanacheza kwa uelewano wa juu tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Tangu kuwasili kwa Kopunovic, amekuwa akiwapanga Mkude na Ndemla kwa pamoja katika nafasi hiyo ya kiungo. Awali alipokuwa kocha Patrick Phiri alikuwa akiwapanga Mkude na Shabaan Kisiga ama Awadhi Juma.
“Kwa sasa tunacheza vizuri, aina yetu ya uchezaji pia inafanana kiasi, nadhani tunapoendelea kucheza pamoja tutaendelea kuzoeana zaidi,” alisema Mkude baada ya timu yao kuifunga Ndanda FC mabao 2-0 juzi Jumamosi.
“Kuhusu mchezo ulikuwa asilimia 50 kwa 50, hatukuwazidi sana lakini tuliweza kuzitumia nafasi tulizopata
vizuri, Ndanda ni wazuri pia na wanacheza vizuri.”
Comments
Post a Comment