KINGUNGE; WANAOTAKA KUOGOMBEA URAIS HAWANA SIFA
Kingunge Ngombale - Mwiru
Harakati za kuwania urais ndani ya CCM zimeingia katika hatua mpya baada ya mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale - Mwiru kuibuka na kudai kuwa wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hawana sifa kwa kuwa wanatumia fedha kutaka kuingia Ikulu.
Kauli ya mwanasiasa huyo ambayo imekuja siku moja kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana leo mjini Unguja na moja ya ajenda ikitajwa kuwa suala la maadili, inaweza kuwa mwiba mchungu kwa wanasiasa hao ambao wanaongezeka kila kukicha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kingunge alisema: “Kuna suala la kukosa uadilifu, kuna suala la matumizi ya pesa na nikwambie ukweli, hao wanaotangaza urais wote wanatumia pesa, wanatumia faulo mbalimbali na wananchi wanajua.”
Kwa miezi kadhaa sasa, baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakitajwa kufanya harakati kichinichini na wengine kushiriki shughuli za wazi zinazoashiria kuwa wanataka kuwania nafasi hiyo ya juu. Hadi sasa makada wanne tayari wameweka wazi nia yao hiyo.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kwa nyakati tofauti walitoa kauli zinazowashutumu makada wengine wa chama hicho kwa matumizi makubwa ya fedha katika kushawishi uungwaji mkono.
Hata hivyo, kauli za wanasiasa hao zimedaiwa kuwa ni fitina za kisiasa kwa kuwa wagombea wote wanatoa fedha, bali wanazidiana viwango tu.
Mbali na Makamba na Membe, wanaCCM wengine waliotangaza au kutajwa kuwania urais ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Kauli ya Kingunge aliyoitoa kupitia Televisheni ya ITV, imekuja wakati wanasiasa sita miongoni mwa hao wanaotajwa wakikaribia kumaliza miezi 12 ya uangalizi kutokana na onyo kali dhidi yao lililotolewa na Kamati Kuu ya CCM Februari 18, mwaka jana baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya “kuanza kampeni mapema na kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya chama na ya jamii.”
Wanaotumikia adhabu hiyo ni Lowassa, Sumaye, Njeleja, Makamba, Wasira na Membe.
Akisisitiza hoja yake hiyo bila kutaja majina, Kingunge alisema makada hao wamekuwa wakitumia fedha nyingi kujitangaza na kutengeneza ushawishi wa kukubalika kwa wananchi jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uongozi.
Comments
Post a Comment