WAZIRI MKUU WA SERIKALI YA WANAFUNZI UDOM AFUKUZWA CHUO MOJA KWA MOJA
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeazimia kumfukuza chuo moja kwa moja waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi Philipo MWAKIBINGA na kumsimamisha Rais pamoja na Katibu wa serikali hiyo.
Maazimio hayo yanafuatia kikao cha Baraza la chuo kilichoketi jana jioni na waliosimamishwa ni Kyabwene (Rais) na Ismail Chande (Katibu)
Viongozi hao wanadaiwa kuchochea mgomo uliotokea jana chuoni hapo, uliohusisha maandamano yaliyofanywa na wanafunzi wa stashahada ya ualimu kupitia mpango maalum wa serikali kwa madai ya kuongozewa posho ya kujikimu pamoja na madai ya kucheleweshewa posho ya chakula.
Kwa upande wake Mwakibinga amekiri kupokea barua ya kufukuzwa chuo na kuongeza kuwa baada ya kukabidhiwa barua hiyo ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka polisi walikokuwa wanashikiliwa tangu jana, alitakiwa kutoka nje ya maeneo ya chuo kuanzia muda huo na alisindikizwa na polisi hadi nje ya maeneo ya chuo.
Amesema hatachoka kupigania ukweli na ataendelea kupigania haki za wanyonge mahali popote atakapokuwa.
Akizungumzia na paparazi kuhusu tuhuma za kuchochea maandamano chuoni hapo, Mwakibinga amesema kuwa yeye kama kiongozi alikuwa analazimika kuwasemea wanafunzi hao ambao bado wako katika hali mbaya kutokana na kutokuwa na pesa ya kujikimu kiasi cha kukosa pesa ya chakula na kula "makombo ya mgahawani".
MWAKIBINGA aliwahi kusimamishwa chuo kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuruhusiwa kurudi chuoni na kuendelea na masomo.
Comments
Post a Comment