SHY-ROSE BHANJI ADAIWA KUMPIGA MBUNGE MWENZIE JIJINI NAIROBI

            Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji ameingia katika mgogoro mpya baada ya kutuhumiwa kumpiga mbunge mwenzake kutoka Tanzania, Dk Nderakindo Kessy jijini Nairobi, Kenya.
Bhanji, ambaye amekuwa katika mgogoro na wabunge wenzake kwa kipindi cha miezi miwili sasa, anadaiwa kumvamia Dk Kessy na kumpiga mgongoni. Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Dk Kessy alisema tukio hilo lilitokea bungeni juzi jioni baada ya kikao kuahirishawa.
“Kwa kuwa muda wa Bunge ulikuwa umeisha nisingeweza kuipeleka kesi hiyo bungeni badala yake ikawa shambulizi na niliambiwa kiutaratibu nikaripoti Kituo cha Polisi cha Bunge ambako baadaye nilikwenda na kupatiwa cheti cha matibabu,” alisema Dk Kessy.
Alisema baada ya kupatiwa cheti cha matibabu na polisi alikwenda katika Hospitali ya AAR jijini humo ambako alipimwa na kupewa majibu aliyoyapeleka polisi kwa uchunguzi.
Hadi tukio hilo linatokea, alisema hakuwa amekwaruzana na Bhanji zaidi ya kushangaa akimvamiwa.
“Baada ya kunipiga hakukuwa na madhara ya papo kwa papo kama alama yoyote mwilini au damu ila nayasikia maumivu, sijui hapo baadaye,” alisema Mbunge huyo ambaye ni kada wa NCCR-Mageuzi.
Bhanji hakupatikana jana kuzungumzia tuhuma hizo, kwani simu yake ilikuwa imezimwa na hata ujumbe wa barua pepe alioandikiwa hakurudisha majibu. Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Eala, Bobi Odiko alisema: “Nimesikia kwamba mmoja ya wabunge alimpiga mwenzake ‘kipepsi’ lakini ilikuwa nje ya Bunge, bado ninaendelea kutafuta ukweli wa kina juu ya tukio hilo.”
Bunge la Eala, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, limekuwa likitawaliwa na vioja na mivutano ya hapa na pale na mikakati ya kumng’oa Spika Magreth Zziwa kwa madai ya kutofanya kazi kwa weledi.
Hivi karibuni, Bhanji aliliingiza Bunge hilo katika mvutano baada ya kudaiwa kuliaibisha wakati wa ziara ya Ubelgiji iliyowashirikisha wajumbe wa tume na wenyeviti wa kamati za Bunge hilo.
Alituhumiwa kufanya fujo ndani ya ndege kwa kutoa lugha chafu kwa wabunge wenzake na matamshi yasiyo ya staha katika hafla iliyoandaliwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Dk Diodorus Kamala.
Baada ya tukio hilo, baadhi ya wabunge walitaka Bhanji achukuliwe hatua za kinidhamu.
Hali hiyo ilifanya vikao vilivyokuwa vikifanyika jijini Kigali, Rwanda mwezi uliopita kuahirishwa kila baada ya dakika 20 au 30 kutokana na wabunge kutumia kanuni ya 31 kutoa hoja zao kutaka mjadala kuhusu Bhanji ufanyike kwanza kabla ya kuendelea na kazi nyingine.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA