EMERSON KUZIBA PENGO LILILOACHWA NA JAJA BAADA YA KUKATISHA MKATABA
Geilson Santana Santos ‘Jaja’
KLABU ya Yanga inatarajia kumsajili kiungo mkabaji mpya kutoka Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe kuziba nafasi hiyo iliyoachwa na mshambuliaji Geilson Santana Santos ‘Jaja’ aliyekatisha mkataba wake na klabu hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Taarifa kutoka Mtandao wa klabu hiyo umesema Emerson De Oliveira Neves Rouqe '24' atawasili nchini Jumanne mchana kwa ajili ya majaribio na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na kikosi cha mabingwa hao mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Kabla ya kuamua kuja Tanzania, Emerson alikuwa akiichezea timu ya Bonsucesso FC inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.
Jaja mfungaji wa mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Azam FC, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 14 alisaini mkataba wa miaka miwili na Yanga akitokea timu ya Itabaina FC na ameichezea timu hiyo kwa miezi minne na kufunga mabao matano katika mechi zote alizoichezea timu hiyo zikiwemo za mashindano na kifariki.
Jaja aliifungia Yanga bao la kwanza ilipocheza mechi ya kirafiki kujiandaa na msimu kwenye uwanja wa Gombani Pemba dhidi ya Chipukizi na kisha alifunga bao lake la pili katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Thika United ya Kenya lakini mashabiki na baadhi ya viongozi wa Yanga hawakuwa wakifuraishwa na kiwango chake.
Mshambuliaji huyo alionekana kuwapa matumaini mashabiki wa Yanga baada ya kufunga mabao mawili safi katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya bingwa mtetezi Azam FC huku bao la pili akilifunga kwa ustadi mkubwa na kuwaziba mdomo mashabiki waliokuwa wakimdhihaki baada ya hapo mechi za Ligi Kuu zilianza na ukame wa mabao ukatawala sana kwake ikiwa ni pamoja na kukosa mkwaju wa penalti katika mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamuhuri mkoani Morogoro.
Staa huyo aliibuka tena katika mechi ya nne ya Ligi dhidi ya Stand United ya Shinyanga kwa kufunga bao lake la kwanza katika ligi na la mwisho baada ya hapo mashabiki hawakuwa wakifurahia anapopewa nafasi uwanjani na kocha raia mwenzake wa Brazili, Marcio Maximo.
Comments
Post a Comment