NDUMBARO AMFUNUA MALINZI TFF
Jamal Malinzi
SAKATA la Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kumfungia Mwanasheria, Damas Ndumbaro kwa miaka saba, limechukua sura mpya baada ya Ndumbaro kupinga kifungo hicho huku akifichua kile alichodai ni ubadhirifu mkubwa wa fedha za wadhamini uliofanywa na shirikisho hilo.
Ndumbaro jana Ijumaa alitumia dakika 37 kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali huku akisisitiza kwamba ameshakata rufaa tangu Oktoba 21 na alidai kwamba uamuzi wa TFF kumfungia unatokana na uamuzi wake wa kusimama haki za klabu za Ligi Kuu Bara.
“Wakati klabu zinanipa kazi hii ya kuwatetea kwenye makato yao ikumbukwe kwamba hoja ya kunipa jukumu hilo ilitoka Yanga ambayo hapa TFF wanasema wanatilia shaka, lakini kabla ya kukubali kutetea klabu nilitaka zote zikubaliane kimaandishi na wote wakasaini kasoro Stand United,”alisema Ndumbaro.
“TFF hawana mamlaka ya kunifungia nilikuwa pale nikitekeleza kazi yangu ya sheria kupitia kampuni yangu ya Maleta & Ndumbaro Advocate na sio kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba wala Mjumbe wa Bodi ya Ligi.
“Nakumbuka wakati tumekutana klabu, TFF na bodi ya ligi Naibu Waziri Juma Nkamia alitamka mbele ya kikao kile kwamba kitendo cha kutaka kuzikata klabu Sh100 katika kila tiketi huo ni wizi wa mchana sasa tafsiri ya adhabu hii ni sawa ni kutaka kunyamazisha kwamba wizi wa mchana uendelee na sitokubaliana na hili nitazitetea klabu,”alisisitiza.
Aidha Ndumbaro alisema sababu kubwa ya TFF kulazimisha kwa nguvu makato hayo ni kutaka kuziba pengo la ubadhilifu mkubwa wa fedha za wadhamini wa Taifa Stars, Kilimanjaro, ambapo mpaka sasa kiasi cha Dola 159,140 (Sh266 milioni) zinaonekana amelipwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Lakini jana Malinzi alipobanwa na Mwanaspoti hakuwa tayari kutoa ufafanuzi wowote kwa madai kwamba leo Jumamosi atatoa tamko la jumla kwa umma.
“Uchunguzi unaonyesha hakuna kielelezo kinachoonyesha fedha hizo zimekwenda kufanya nini, hawa jamaa walitumia siku mbili kunifungia, lakini tangu nimekata rufaa Oktoba 21 nikiwa Marekani mpaka leo (jana) hakuna kilichosikilizwa,” alisema.
Comments
Post a Comment