PHIRI AMPA MAXIMO MECHI TATU


Kocha wa timu ya Yanga Mbrazil Maxio Maximo (kulia) akiwa na kocha wa Simba Patrick Phiri


KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri ametamka kauli ambayo huenda ikawalainisha mashabiki wengi wa timu hiyo wenye hasira na matokeo ya sare sita mfululizo. Maneno hayo pia ni mkwara kwa Yanga ya Marcio Maximo na Azam ya Mcameroon, Joseph Omog.
Phiri amewaambia Simba kwamba suluhisho la hali ya sasa ni dogo sana na likishafanyika kila mtu atanyamaza kimya na Simba itarejea kwenye hadhi yake na itaongoza ligi kwavile Yanga na Azam zimeanza kupotea njia na zinapoteza mechi wakati yeye hajapoteza.
Ni hivi; Phiri anataka kushinda mechi tatu mfululizo na kwa idadi ya mabao matatu au zaidi ndio maana jana Jumatatu asubuhi amewarudisha wachezaji ufukweni.
Kocha huyo anasema kwamba akishinda mechi hizo atakuwa amefikia pointi za timu zilizoko kileleni kwa sasa na wakifunga idadi ya mabao hayo hata kama timu itaendelea kuyumba hayawezi kurudi yote kirahisi kipindi cha pili na Simba itashinda.
Phiri alisema: “Tofauti yetu na wanaoongoza ligi ni pointi nane hapo ni sawa na kusema tutakaposhinda mechi tatu mpaka nne Simba inaweza kuongoza ligi na hilo linawezekana angalia uwezo wa wachezaji katika mechi yetu iliyopita dhidi ya Mtibwa, naweza kusema bao lao walilopata ni kama tulijifunga kutokana na makosa yetu .”
“Mimi sihofii kufukuzwa hapa, watu waelewe Phiri sio mtu muhimu kuliko timu na unapozungumzia timu ni kocha, wachezaji, viongozi na mashabiki kama kocha natimiza wajibu wangu, kila mtu akifanya hivyo Simba inaweza kuondoka hapa ilipo, hiki ni kipindi kigumu kinachopita hakiwezi kukaa msimu mzima.
“Tukishinda mechi ijayo na zingine mbili msimamo wa ligi hauwezi kuwa kama ulivyo sasa tunaweza kuwa juu ya Yanga, Azam na hata Mtibwa kama wakipunguzwa kasi, kutokana na tofauti iliyopo sasa hakuna anayefurahia hali hii ndani ya Simba, angalia wachezaji walivyoumizwa na matokeo yaliyopita kiasi cha kutoa machozi hii ni ishara kwamba wanapambana,”alisisitiza Phiri.
“Tumeumizwa na sare sita mfululizo, siyo jambo zuri na hakuna anayetaka iwe hivyo, kikosi kwa sasa kimeimarika hivyo tunatafuta tu fomula ya kupata ushindi kwa sasa maana uwezo tunao.Nataka washambuliaji wangu waongeze juhudi kwenye mechi hizo, nataka wafunge mabao mawili, matatu ama zaidi, hii itakuwa ngumu kwa wapinzani wetu kurudisha, hii itatusaidia kupata ushindi hata kama tutafanya makosa,” alisema Phiri.
Hata hivyo kocha huyo amesema anafurahi kuona ligi inasimama baada ya mechi saba kwani ingeenda hadi mechi 13 kama msimu uliopita basi hali ya kikosi chao ingekuwa mbaya zaidi.
“Ni jambo jema ligi inasimama baada ya mechi saba tu, zingekuwa hizo 13 tungekuwa na hali mbaya, ligi ikisimama tutapata wasaa mzuri wa kujiandaa na kurekebisha makosa yetu, tutapata pia fursa ya kusajili wachezaji tunaowahitaji,” alisema Phiri.
SIMBA UFUKWENI

Phiri jana aliamua kubadilisha mazoezi ya uwanjani na kuwapeleka wachezaji wake ufukweni kwa ajili ya mazoezi ya utimamu wa mwili, ambapo amesema huenda mazoezi hayo yanaweza kubadilisha matokeo kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA