KIMBUNGA DIKELEDI KUIKARIBIA TANZANIA, WAKAZI WA MAENEO HAYA WAPEWA TAHADHALI



Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa rasmi kuhusu kimbunga Dikeledi kinachopitia Bahari ya Hindi karibu na pwani ya Msumbiji. Kwa mujibu wa tathmini ya hali ya hewa iliyofanywa, kimbunga hicho hakina athari za moja kwa moja kwa upande wa Tanzania, lakini kinaweza kuleta vipindi vya mvua kubwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

TMA imeeleza kuwa kimbunga Dikeledi, ambacho kwa sasa kipo mwambao wa Msumbiji, kinatarajiwa kurejea katika Rasi ya Msumbiji leo alasiri. Ingawa hakitathiri moja kwa moja maeneo ya Tanzania, ukaribu wake na pwani ya kusini unatoa uwezekano mdogo wa kuibuka kwa mvua kubwa na upepo mkali.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari vinatarajiwa kuathiri ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi kati ya Januari 14 na 15, 2025. Hali hii inaweza kuwa changamoto kwa shughuli za uvuvi na usafirishaji wa majini, hivyo basi watumiaji wa bahari wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi hiki.

TMA ilianza kutoa tahadhari ya hali ya upepo mkali kuanzia Januari 11, 2025, huku ikieleza kuwa hali hiyo inatarajiwa kutulia ifikapo Januari 16, 2025. Mamlaka hiyo imewahimiza wananchi kufuatilia kwa makini mabadiliko ya hali ya hewa kupitia vyanzo rasmi ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea maeneo hayo.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga Dikeledi na athari zake kupitia mifumo ya hali ya hewa nchini. Ambapo wananchi wanashauriwa kuwa makini na kupata ushauri wa kisekta ili kuhakikisha usalama katika shughuli za kila siku, hasa katika maeneo yanayoweza kuathirika.

Je, wewe ni miongoni mwa watu wanaoishi katika maeneo tajwa au karibu na maeneo tajwa? Chukua tahadhari, pia endelea kuwa karibu na vyanzo vya taarifa vya TMA.

Chanzo: Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA