KASEJA AMPA SHARTI GUMU MAXIMO
YANGA imebakiza mechi nane kabla ya kukamilika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara lakini meneja wa kipa wa timu hiyo Juma Kaseja ameutahadharisha uongozi wa klabu hiyo kwamba mchezaji huyo asipochezeshwa mechi tatu kati ya hizo atamtoa Jangwani.
Abdulfatah Saleh ambaye ndiye meneja wa Kaseja ameliambia Mwanaspoti kuwa hawafurahii matumizi ya kipa huyo katika kikosi hicho ambapo bado wanaimani kwamba Kaseja ni kipa bora hapa nchini.
Abdulfatah alisema kwa sasa katika mechi nane za Yanga wataangalia nafasi ya Kaseja katika kikosi hicho na endapo atashindwa kudaka mechi zisizopungua tatu katika timu hiyo watalazimika kufanya uamuzi mgumu.
“Mimi kama meneja wake sikubaliani na mteja wangu anavyoishi ndani ya Yanga, hapati mechi za kutosha na kudaka tumefuatilia mazoezini tumegundua kwamba Kaseja ana juhudi kubwa za kudaka na anafanya vizuri hata wachezaji wenzake baadhi wanashangaa ni kwanini hadaki,” alisema.
“Hatutaki kuingilia kazi ya kupangwa timu yao lakini kwetu tutaangalia jambo moja endapo kocha wao atashindwa kumpanga Kaseja katika mechi tatu kati ya nane zilizosalia mwisho wa mzunguko wa kwanza tutalazimika kuangalia upya uwepo wa kipa huyo Yanga.
“Kaseja bado ni kipa ambaye ana uwezo mkubwa wa kudakia klabu yoyote hatufurahii kuona anajituma mazoezini na kupewa mechi za kirafiki, ni kama vile kuna watu wachache ambao wameamua kuleta mzaha na kipaji chake,”alisema bosi huyo ingawa habari za ndani zinadai ana mpango wa kumpeleka Simba endapo Yanga watashindwa kufuata masharti ya mkataba.
Haijulikani kama kocha wa Yanga, Marcio Maximo ataridhia masharti ya kutakiwa kumpanga Kaseja ili asiondoke.
Comments
Post a Comment