MKWASA AANZA YAKE TAIFA STARS
KOCHA Mkuu mpya wa Taifa Stars, Boniface Mkwasa, ameanza yake baada ya kutangaza benchi lake la ufundi sambamba na kikosi kipya cha timu hiyo akiwajumuisha kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ na Samuel Kamuntu ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa mchezaji huyo wa JKT Ruvu kuitwa Stars.
Mkwasa alitangaza jopo lake jipya jana Jumatano ambalo linawajumuisha Juma Mgunda, Abdallah Kibadeni, Hemed Morocco na Peter Manyika.
Mgunda ameteuliwa kuwa Meneja wa timu hiyo, huku Manyika akiwa ni Kocha wa Makipa wakati Morocco anakuwa Kocha Msaidizi na Kibadeni ni Mshauri wa timu na mtunza vifaa ni Hussein Sued ‘Gaga’ ambapo Mratibu wa timu hiyo anakuwa Ahmed Mgoyi.
Juu ya kikosi kipya cha timu hiyo kinachojiandaa na pambano la marudiano dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezani wa Ndani (Chan) 2016, Mkwasa ameita jumla ya wachezaji 26 ambao ni pamoja na makipa ‘Barthez’ (Yanga), Mwadini Ali (Azam), Mudathir Hamis (KMKM).
Wengine ni mabeki, Shomary Kapombe na Aggrey Morris (Azam), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Hassan Isihaka (Simba), Mwinyi Haji Ngwali, Juma Abdul, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani (Yanga).
Viungo ni Hassan Banda, Jonas Mkude na Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Said Ndemla (Simba) na Salum Telela (Yanga) wakati safu ya ushambuliaji inaundwa na Simon Msuva, Deus Kaseke (Yanga), Rashid Mandawa (Mwadui), John Bocco, Ame Ali, Mudhathir Yahya (Azam), Atupele Green(Kagera Sugar), Ramadhani Singano (Simba) na Kamuntu.
Mkwasa alisema wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini leo katika hoteli ya Tansoma na kesho Ijumaa wataanza mazoezi rasmi nje ya jiji la Dar es Saalam.
Stars itaifuata Uganda kurudiana nayo katika mchezo wa Julai 4 kuwania kufuzu fainali hizo za Chan zitakazofanyika Rwanda mwakani..
Comments
Post a Comment