AFYA YAKO:AFYA YA NGOZI (Sehemu Ya Kwanza).

Na Dr. Richard Zuberi


UTANGULIZI
Tunamshukuru Mungu kwa nafasi nyingine ambayo ametupa kuwepo hai tena na hata kuweza kushiriki darasa letu fupi hapa, pia napenda nimshukuru kila mmoja ambaye amekuwa akishiriki katika meza yetu hapa kwa namna moja ama nyingine, hata kwa kusoma tu na kupita, kufanya kwako hivyo kunanisukuma kuendelea kusema yale machache ambayo kwa sehemu ninayafahamu. Wiki hii tutaanza kuangalia somo la AFYA YA NGOZI, soma kwa faida yako na jirani yako, soma hata kama una allergy (mzio) na maandishi/maandiko.
Ngozi sio kiungo kigeni au kilichojificha kama ulivyo moyo, figo au maini, ngozi ipo nje na kila mtu anaweza kuiona. Ngozi ndiyo kiungo kikubwa kuliko viungo vyote katika mwili wa mwanadamu, ngozi imegawanyika katika sehemu kubwa tatu; ngozi ya nje, ya kati nay a ndani.
KAZI ZA NGOZI
Kulinda mwili mbali na maambukizi ya wadudu wasababishao magonjwa,Kulinda mwili usipoteze maji kama mvuke,Kulinda sehemu za ndani ya mwili zisipate jereha hasa pale ngozi inapojeruhiwa, Kuhifadhi joto la mwili lisipande au lisishuke,Kutengeneza vitamins mf. Vitamin D, Kuhifadhi maji na mafuta, Kutoa uchafu mwilini kama jasho na Kutumika kama mlango wa fahamu, kuleta hisia na muhemko.
TABIA RAFIKI KWA AFYA YA NGOZI
1. Kupenda kunywa maji ya kutosha; maji ni dawa na kinga kubwa sana ya magonjwa ya ngozi na husaidia sana kuzuia ngozi isiwe na mikunjokunjo na kuonekana mzee kabla ya wakati, kuamua kunywa maji kati ya lita 3 hadi tano katika masaa 24 kutakusaidia kuwa na ngozi yenye afya (tutakuwa na siku maalumu ya kutazama umuhimu wa maji ya kunywa)
2. Kupenda kula mlo kamili; vyakula vyenye vitamin mfano vitamin A,C na E vinasaidia sana ngozi yako kuwa na afya, kwa hiyo ni muhimu sana kula matunda, mbogamboga, samaki/dagaa, nyanya, n.k. Ulaji wowote wenye mafuta ya kupitiliza sio rafiki kwa afya ya ngozi.
3. Kufanya mazoezi ya mara kwa mara na yaliyo katika utaratibu; mazoezi yanasaidia kuondoa mafuta yaliyopitiliza yenye athari kwa afya ya ngozi, mazoezi pia husaidia kupunguza “free radicals” ambazo zinachangia ngozi kuwa na makunyanzi na kuonekana mzee kabla ya wakati.
4. Kupata muda wa kupumzika, ngozi kama sehemu ya mwili na ni kiungo kikubwa kabisa katika mwili kinaweza kuwa na afya bora zaidi iwapo utapata muda wa kupumzika, kuamua tu kuwa “bize” kila siku na kukosa muda wa kupumzika ni hatari kwa afya ya ngozi.
5. Kuishi maisha yasiyo na msongo wa mawazo wa kudumu, haiwezekani kuishi bila stress, hata hapa naandika MEZANI KWA TABIBU ya leo nina stress sijiui kama watu wataelewa ninachoandika au nitaongea lugha ya kitaalamu zaidi matokeo yake kuwafurahisha madaktari na manesi watakaosoma ambao hasa sio audience yangu na kuwaacha gizani wale wasio na fani za kitabibu. Huwezi kuishi “stress-free”, asikudanganye mtu (Kuna siku tutaongea hapa kuhusu stress) lakini maisha ambayo kila siku una stress si rafiki kwa afya ya ngozi yako, stress inaongeza free radicals ambazo ni hatari kwa afya ya ngozi, ukiwa full stress unaweza kuona kila siku unabadilisha mafuta, lotion sijui “angel face” lakini uso bado unagoma kabisa na chunusi zinaendelea kupiga hodi.
6. Kuepuka matumizi ya mafuta au vipodozi ambavyo vina kemikali hatarishi kwa afya ya ngozi yako, sio kila mafuta ambayo yamemsaidia mwingine kuwa na ngozi nzuri yatakusaidia na wewe, ngozi zetu zinatofautiana. Kuna ngozi kavu na kuna ngozi yenye unyevunyevu (laini) na matumizi ya mafuta/vipodozi/vipendeza mwili lazima yaendane na aina ya ngozi yako (Hii siingii ndani maana sio mtaalamu wa urembo). Kuna wengine walitumia vitu fulani kwa ajili ya kupendeza matokeo yake wanahangaika kila siku kutibiwa magonjwa ya ngozi.
7. Kuepuka kukaa juani kwa muda mrefu bila sababu ya lazima, ngozi ina utando unaitwa MELANIN ambao unazuia mionzi mikali ya jua isipenye mwilini na kuleta madhara, lakini ukikaa muda mrefu juani unakuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya ngozi.
8. Kuwa na tabia ya usafi tu wa kawaida, kuna watu wengi wana matatizo katika ngozi zao lakini chanzo kikubwa ni UCHAFU tu, kutokuoga au kutokuoga kwa ufasaha, kutosafisha kila sehemu ya ngozi, kuvaa nguo za ndani zisizo safi, kuna wanaume wenzangu ambao wanavaa boksa moja kwa siku tatu, ni majanga.
9. Kuepuka kutumia dawa bila maelekezo sahihi ya daktari.
10. Kuepuka kukaa au kutembea mahali ambapo kuna wadudu hatari kwa ngozi yako
11. Kuepuka kuvaa nguo ambazo hazinyonyi jasho la mwili kwa utoshelevu, hasa nguo za ndani ni vema zikiwa za pamba
12. Kuepuka kutumia muda mrefu karibu na joto (moto) kali/mkali, kuepuka kushika/kukanyaga maji au kemikali hatarishi kwa muda mrefu
13. Kuwahi kupata ushauri wa kitabibu na matibabu sahihi mapema iwezekanavyo baada ya kupata ugonjwa wa ngozi.
……………………….ITAENDELEA JUMATANO IJAYO

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA