JAVU AWAGAWA VIONGOZI YANGA

AKIWA ni mmoja ya wachezaji waliotajwa kutemwa ndani ya klabu ya Yanga, mshambuliaji Hussein Javu amedaiwa kuwagawa viongozi wa timu hiyo pande mbili.
Inaelezwa kuwa dili lake la kutaka kusajiliwa na JKT Ruvu, limemfanya Javu kubaki njiapanda, baada ya baadhi ya viongozi wa Yanga wakitaka apewe mkataba mpya kisha atolewe kwa mkopo, huku uongozi wa maafande ukisema hautaki mchezaji yeyote wa mkopo msimu ujao.
Unajua ilikuaje? JKT Ruvu ilimejitosa kumnasa Javu baada ya kusikia Yanga haina mpango naye, lakini wakiwa kwenye mchakato wa mazungumzo. Javu aliueleza uongozi wa klabu hiyo kuwa Yanga wanataka kumsaini kisha ataweza kujiunga nao kwa mkopo.
Uongozi wa Ruvu ulisikiliza kwa umakini na kudai kuwa wasingeweza kumchukua mchezaji huyo kwa mkopo.
Katibu wa JKT Ruvu, Ramadhani Madoweka alisema, “Tunataka mchezaji ambaye atakuwa wetu jumla, tusingependelea kuwa na mchezaji ambaye anakuja kwa mkopo kwa sababu kujitolea kwao ni kudogo na hii tumekuwa tukiona kwa wachezaji wengi wanaoenda kwa mkopo kwenye timu nyingine.
“Mchezaji yeyote tunayemtaka, basi ajue tutamsajili na si kwamba asajiliwe kwingine kisha aje kucheza kwetu kwa mkopo. Hilo hatutalifanya,” alisema katibu huyo.
Baadhi ya viongozi Yanga bado wanaguna juu ya kuachwa kwa straika huyo wakati wengine wakidai kuwa hana kiwango cha kuendelea kuwepo Yanga.
Hata hivyo Javu alivyotafutwa hakupatikana lakini habari zilizopo ni kuwa Yanga wanataka kumpa mkataba mpya lakini wamtoe kwa mkopo kwenye timu nyingine ili watakapomhitaji waweze kumchukua.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA