BEKI WA ZAMANI AWAPA SOMO WENZAKE BONGO
Aliyekuwa beki wa Simba, David Naftal
BEKI wa zamani wa Simba, David Naftal anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Ushuru ya Kenya, amewaambia wachezaji wenzake nchini ambao wanakosa nafasi kwenye timu zao hasa Simba na Yanga kuiga mfano wa Dan Sserunkuma.
Dan alisajiwa Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo akitokea Gor Mahia ya Kenya akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Kenya (KLP) lakini alishindwa kutamba ndani ya Simba ambapo aliondoka akiwa amefunga mabao matatu pekee huku akipotezewa na kocha Goran Kopunovic.
Sasa Naftali aliwapa akili wachezaji wa Kibongo kwa kuwaambia kwamba wachezaji wengi ndani ya Simba na Yanga hawapati nafasi za kucheza na wanaogopa kuziacha timu hizo kutokana tu na ukubwa wa majina ya timu husika pasipo kujali kushuka kwa viwango vyao.
“Ni kweli katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo inayolipa vizuri lakini je usipocheza hiyo pesa unaitoa wapi, maana najua timu za Simba na Yanga ukicheza ndio maisha yako yanakuwa mazuri, kikubwa wachezaji wajaribu kutoka ili wapate nafasi ya kuendeleza vipaji vyao,” alisema.
“Nampongeza Dan baada ya kuona mambo si mazuri aliamua kujiengua, sio kwamba ni mbaya kisoka ila alikutana na mazingira mapya, timu mpya ambayo ilikuwa katika kipindi kigumu na hawakumpa nafasi ya kumvumilia ili aweze kuendana na soka la Bongo na presha ya timu kama Simba,” alisema Naftali.
Akizungumzia changamoto ya ligi ya Kenya, Naftali alisema; “Ligi ya huku ina changamoto nyingi ya wachezaji kutoka nje karibia timu zote zina wachezaji wa kigeni zaidi ya wanne na zipo chini ya makampuni tofauti na Tanzania ambapo timu chache ndio zina uwezo wa kusajili wachezaji kutoka nje, hivyo unaona kabisa kuwa ligi ni ya upande mmoja.”
Comments
Post a Comment