AJINYONGA BAADA YA KUGUNDULIKA KUWA ANAVIRUSI VYA UKIMWI
MKAZI mmoja wa Mtaa Myegeya katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Mathias Ngimba (41), amekutwa amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia kipande cha nguo kwa kile kilichodaiwa baada ya kupimwa afya yake alibainika kuwa ana maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Akizungumza jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, alisema tukio hilo limetokea Juni 20, mwaka huu saa 4 asubuhi katika nyumba ambayo aliwekwa na kaka yake marehemu aitwaye Festo Ngimba.
Kamanda alisema marehemu Mathias Ngimba, inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa pamoja na tumbo la kuhara ndipo alipochukua maamuzi ya kwenda katika Zahanati ya jeshi iliyopo Chaburuma na kupimwa afya yake ili kubaini tatizo linalomsumbua.
“Marehemu alipofika zahanati alipimwa na kubainika maradhi yanayomsumbua aligundulika kuwa ameshapata maambukizi ya VVU ndipo akarejea nyumbani alipokuwa akiishi na kuamua kuchukua maamuzi wa kujinyonga kwa kutumia kipande cha nguo.
“… alijingonga huku akiwa ameacha ujumbe uliosomeka kuwa ameamua kujitoa duniani kwa hiyari yake mwenyewe ili asiisumbue Serikali pamoja na ndugu zake,” alisema Kamanda Msikhela.
Kutokana na tukio hilo Kamanda huyo wa polisi amewataka wananchi kuachana na tabia ya kujihukumu kwa kujitoa uhai kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Comments
Post a Comment