MMILIKI WA IPTL ATEMA CHECHE



Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh
Dar/Mikoani. Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habirnder Seth Singh amesema anafikiria mara mbilimbili iwapo aendelee kuwekeza nchini au la, baada ya kuwapo kwa tuhuma kwamba alihusika na uchotaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Nimeongelewa sana kiasi kwamba naona kama hakuna hata amani ya kuwekeza Tanzania, nitajifikiria mara mbili mbili. Wananchi wanaelewa vingine kabisa kuhusu suala hili kwa sababu ya upotoshwaji,” alisema Singh alipozungumza na gazeti hili jana.
Singh ambaye alituhumiwa kujipatia asilimia 70 ya hisa katika Kampuni ya IPTL isivyo halali, alisema hafikirii kuwekeza zaidi nchini kwa sababu yamekuwapo maneno mengi na shutuma zisizo na ukweli zilizoelekezwa kwake kuhusu sakata hilo.
Kauli ya bosi huyo wa IPTL imekuja wakati Taifa likisubiri utekelezaji wa maazimio ya Bunge na akiwa mmojawapo wa watu wanaotakiwa kuchunguzwa na vyombo vya dola ili akibainika kufanya makosa, afikishwe mahakamani.
Jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza haraka maazimio manane yaliyotolewa na Bunge dhidi ya ufisadi wa sakata la escrow.
“Rais hatakiwi kukaa kimya, atoe tamko la haraka ili kuwaondoa viongozi hao. Hata Waziri Mkuu anatakiwa kuwajibishwa kwa sababu ni chanzo cha udhaifu huo,” alisema Profesa Lipumba alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF (JUKECUF).
Jana, Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema alisema: “Kwangu ni kama hukumu imetangulia mashtaka kwa sababu sikuwahi kuitwa kuhojiwa mahali popote, ila ninauheshimu uamuzi wa Bunge.”
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema hayuko tayari kuzungumzia masuala ya kashfa ya Akaunti ya Escrow pamoja na mwingiliano wa mihimili miwili, Bunge na Mahakama kwa kuwa siyo wakati wake.
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa Benki ya Stanbic Tanzania nao ulitoa taarifa ya kukana kuhusika katika utakatishaji fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya Bunge kupitisha azimio la kuitaka mamlaka husika za kifedha kuichunguza.
Malamiko ya Singh
Singh alisema kampuni yake imekuwa ikiuza umeme kwa bei nafuu; senti nane kuliko kampuni nyingine, lakini bado anaonekana kuwa na makosa.
“Kuuza umeme kwa senti nane kwa megawati ni bei nafuu sana lakini mbona naonekana kama nina makosa? Ndiyo maana ninasema nitafikiria mara mbili kuwauzia umeme,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA