IVO, MATOLA WAKUNJANA


                    kipa wa Simba,Ivo Mapunda 

HALI ya kambi ya Simba iliyopo kisiwani Unguja, Zanzibar si shwari baada ya Kocha Msaidizi, Seleman Matola na kipa Ivo Mapunda, kutaka kurushiana makonde baada ya kutofautiana kauli walipokuwa wakitafuta suluhu ya tofauti zao za muda mrefu.
Habari kutoka kambini humo zinadai kuwa wawili hao juzi Jumanne walitofautiana kauli baada ya mazoezi ya asubuhi na kuzuka ugomvi ulioamuliwa na kocha Patrick Phiri kwa kuwataka wakae pembeni na kumalizana kiutu uzima, baadaye walisuluhishwa na mratibu wa kambi hiyo, Abdul Mshangama.
Chanzo cha habari kiliendelea kusema kwamba ugomvi wa Matola na Mapunda ulianza tangu kipindi ambacho Mapunda aliumia kidole walipokuwa kambini wakijiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara na juzi Mapunda alishindwa kuuvumilia na kutaka suluhu. Imeelezwa kuwa Matola alikuwa akimshutumu pia Mapunda kuwa amekuwa akiruhusu mabao mepesi jambo linaloigharimu timu hiyo kitu ambacho Mapunda hakukubaliana nacho. Tuhuma hizo ziliendelea mpaka baada ya mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ilipofungwa bao 4-2.
Mwanaspoti lilimtafuta Ivo ambaye alikiri kuwepo na tofauti hizo, lakini alikanusha uvumi wa kupigana na kocha wake, huku akiweka wazi kuwa yeye na Matola walikuwa hawapatani kwa muda mrefu sasa.
“Naomba watu na mashabiki wa Simba waelewe wazi kuwa mimi na Matola hatujapigana, huo ni uvumi tu bali tulitofautiana kauli katika maongezi hali ambayo ilipelekea tuzozane na siyo kupigana,” alisema.
“Chanzo cha haya yote ni kwamba mimi na Matola tulikuwa hatupatani kwa muda mrefu, sidhani kama watu wengi wanafahamu hilo, lakini niliona si vyema kuendelea kuishi maisha kama haya wakati tunafanya kazi moja ya mpira japokuwa yeye ni kocha wangu, kwani mpira una mwisho wake na tunaweza kukutana mtaani.
“Nilimweleza kocha Phiri (Patrick) kuwa nahitaji suluhisho la hili suala mbele ya kikao cha wachezaji ili liwe wazi kwani nao wanafahamu, lakini kocha alikataa na kudai kuwa tuzungumzie pembeni ikawa hivyo, nilimweleza Matola dukuduku langu, lakini nafikiri hakunielewa namaanisha nini ndiyo maana akanijia juu.
“Hapo ndipo kuzozana kulipoanzia, lakini naamini Matola hakunielewa, hivyo hatukufikia suluhisho lolote ndipo alipoelezwa Mshangama ambaye alituita baada ya mazoezi ya jioni, tulikaa pamoja na kuzungumza huku kila mmoja akieleza yake, tumepatanishwa na sasa hakuna tofauti yoyote. Ninamheshimu kama kocha na yeye ananiheshimu kama mchezaji, haya ndiyo maisha ninayoyahitaji kwa sasa.”
Kwa upande wake Mshangama alisema: “Ni kweli kulikuwepo na tofauti kati ya Ivo na Matola, hii ni tangu kipindi hicho Ivo alipoumia, inadaiwa kuna maneno mabaya Matola alizungumza juu ya kuumia kwa Ivo ambayo hayakumfurahisha mwenzake, sasa jana (juzi Jumanne) Ivo alikuwa anataka suluhu baada ya mazoezi ya asubuhi.
“Walibishana tu lakini hawakupigana.”
Mwanaspoti ilipomtafuta Matola ili naye azungumzie suala hilo, simu yake ilikuwa ikiita tu bila ya kupokewa.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA