DAN SSERUNKUMA ASAINI MIAKA MIWILI SIMBA



            Simba wakipata chakula 

UMEONA mambo hapo ukurasa wa mbele? Mnyama katisha. Amemsainisha straika namba moja wa Gor Mahia ya Kenya, Mganda Dan Sserunkuma, mkataba wa miaka miwili na kufanya Simba iwe na mastraika wanne wa maana.
Usajili huo ni imara kuliko ule wa Yanga ambayo mpaka sasa haijasajili straika yeyote wa maana baada ya kumtema Mbrazili Genilson Santos ‘Jaja’.
Yanga inamtegemea nchini muda wowote straika wa Zambia ambaye atakuja kufanyiwa majaribio na akikubalika huenda akapewa nafasi ya Hamis Kiiza ambaye ni mshambuliaji wa Uganda aliyeshindwa kumshawishi Marcio Maximo kwenye kikosi cha kwanza. Yanga ina mastraika wanne ambao ni Kiiza, Jerry Tegete, Husein Javu na Said Bahanuzi.
Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri, amesema kuwa ujio wa Sserunkuma ni mpango wa kuhakikisha kuwa kuna ushindani kwenye nafasi ya ushambuliaji ya kati na kusema kuwa mifumo atakayokuwa akitumia itahitaji straika mmoja pekee hivyo ni muda wa mastraika hao kuwania nafasi.
Phiri alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuleta ushindani kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati na ambayo ina Elius Maguli, Amissi Tambwe na Sserunkuma.

“Nina mastraika watatu wa kati, nafasi yao kwenye kikosi ni moja tu hivyo wanatakiwa kuchuana na kuhakikisha wanapata nafasi, nitahitaji straika mmoja wa kati,”alisema kocha huyo.
Nahodha wa Simba, Joseph Owino, ambaye ni raia wa Uganda aliliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka kwao akisema: “Ujio wa Sserunkuma utatusaidia ukizingatia kuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye kasi ya ajabu.
“Mtamuona kwenye mechi dhidi ya Yanga na naamini kwa staili yake ya uchezaji ataisumbua safu ya ulinzi ya Yanga.
“Nawajua sana (Kevin) Yondani na Cannavaro (Nadir Haroub) kwa ubora wa kucheza mipira ya juu, lakini Sserunkuma ni mchezaji mwenye kimo cha kawaida na huwa hashindani na mchezaji kwenye kuwania mipira ya juu, mara kadhaa nilikuwa namtazama kwenye Ligi ya Kenya na timu ya Taifa, kuwa ni mtu anayependa kucheza mpira wa chini.”
Usajili wa dirisha dogo utamalizika Desemba 15 lakini Yanga wamepanga kufanya mambo kimyakimya mpaka dakika za mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

JINSI YA KUKAA NA NGUVU ZA MUNGU SEHEMU YA KWANZA